.

.
Friday, May 2, 2014

3:24 AM
SHEREHE za Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) mkoani Arusha zimetawaliwa na hotuba kuhusu milipuko ya mabomu iliyosababisha vifo vya watu na kuwaacha wengine na ulemavu wa kudumu.
Hotuba hizo zilitolewa na wafanyakazi wa sekta mbalimbali kabla ya kuhitimishwa na risala ya Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo.
Kabla ya kuanza kwa hotuba za wafanyakazi, maandamano ya magari ya taasisi na makampuni mbalimbali yalipita mbele ya mkuu huyo wa mkoa huku hospitali ya mkoa, Mount Meru wakipita na gari la wagonjwa wakiigiza bomu kulipuka mahali na kusababisha kifo cha mtoto na kuacha majeruhi kadhaa.
Licha ya kuigiza hali hiyo, walitoa wito kwa watendaji kudhibiti isitokee tena huku wakiwataka wadau kujitokeza kuisaidia hospitali hiyo kukabiliana na majanga ya aina hiyo, hasa kuhudumia majeruhi wa milipuko ya mabomu.
Hotuba ya wafanyakazi iliyosomwa na Katibu Mkuu wa RAAWU mkoani hapa, Mary William, ilieleza jinsi wafanyakazi wanavyokumbwa na hofu ya mabomu kila kukicha, hivyo kuwafanya washindwe kuongeza tija katika utendaji wao.
“Tunashauri mgambo wengi waliohitimu mafunzo watumike ipasavyo katika ulinzi wa maeneo ya mitaani, ambako wanaishi ili kudhibiti matukio kama hayo tofauti na sasa ambapo mgambo wapo wengi, lakini kunakotokea milipuko ya mabomu hakuna kinachoendelea,” alisema Mary.
Kwa upande wake, Mulongo alizungumzia matukio hayo na kusema uchunguzi wa mashirika ya kimataifa ikiwemo Interpol unabainisha kwamba matukio hayo si ya kigaidi bali na mabomu ya kutengenezwa.
“Hao wataalamu wa kimataifa tulioshirikiana nao wanasema wazi kuwa tujiangalie sisi wenyewe hapa Arusha kwani matukio hayo hayana uhusiano na ugaidi, hivyo ni wajibu wetu kusimamia ulinzi ili kuepuka mabomu,” alisema Mulongo.
Akizungumzia msingi wa sherehe yenyewe, Mulongo alitoa wito kwa watendaji wa serikali kufanya kazi kwa bidii ili wananchi waone na waridhike kila mmoja katika sekta yake kuhakikisha huduma wanazotakiwa kuzitoa kwa wananchi wanazipata bila vikwazo.

0 comments:

Post a Comment