.

.
Sunday, May 11, 2014

10:01 PM
SHARE THIS STORY
0
Share

Dodoma. Uzalishaji wa chakula Ukanda wa Nchi za Afrika Mashariki, unatarajiwa kuongezeka msimu wa kilimo wa 2014/2015, hivyo kupunguza soko la mazao ya chakula yanayozalishwa nchini.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza alisema kama hali itakuwa hivyo, Serikali inawashauri wakulima na wafanyabiashara nchini kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2014/2015 bungeni jana yanayofikia Sh318.7 bilioni, Chizza alisema wakulima na wafanyabiashara wataruhusiwa kuuza mazao nje ya nchi.
Chizza alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa, mvua zimenyesha vizuri katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, hali inayoashiria kuwapo kwa mavuno mazuri katika nchi hizo.
Kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikizuia mazao ya chakula, hususan mahindi ambayo yana soko kubwa nchi za Kenya na Somalia kuuzwa nje.
“Hali ikiwa hivyo kwa maana ya kuongezeka mavuno nchi nyingine za Afrika Mashariki, Serikali inawashauri wakulima na wafanyabiashara kutafuta masoko nje ya nchi,” alisema Waziri Chizza na kuongeza:
“Napenda kusisitiza kwamba, Serikali haizuii uuzaji halali wa chakula cha ziada nje ya nchi kwa sababu tunatarajia kupata mavuno mengi msimu huu wa kilimo,” alisema waziri huyo katika bajeti yake.
Hata hivyo, Waziri Chizza alisema hali halisi ya chakula kitakachovunwa nchini msimu huu wa kilimo itajulikana baada ya kufanya tathmini Juni, 2014.
Alisema ingawa dalili ziko hivyo, lakini watakuwa na uhakika zaidi wa hali ya chakula kufikia katikati ya mwaka huu.
Wakati huohuo, Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), imepanga kununua kutoka kwa wakulima tani 200,000 za nafaka, zikiwamo tani 190,000 za mahindi na tani 10,000 za mpunga kwa msimu wa kilimo wa 2014/2015.

0 comments:

Post a Comment