MKAKATI wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) wa kupeleka madaraka kwa wananchi kupitia kanda
kumi za kichama zilizoundwa na Baraza Kuu hivi karibuni umeanza kazi
rasmi kwa kila kanda kuweka mikakati yake.
Katika mgawanyo huu, Kanda ya Kaskazini ilipangwa kuwa na mikoa ya
Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara ambapo Mkoa wa Arusha
ulichaguliwa kuwa makao makuu ya Kanda ya Kaskazini.
Taarifa ya kanda hiyo kwa vyombo vya habari jana ilisema kuwa,
Februari 16 na 17 mwaka huu, kutakuwa na kikao cha kwanza cha chama
Kanda ya Kaskazini ambacho kitajumuisha wabunge wote kutoka mikoa ya
kanda hiyo akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Freeman Mbowe na
viongozi wa chama wa mikoa.
Kwamba kikao hicho pia kitahudhuriwa na wenyeviti na mameya wa
halmashauri zinazoongozwa na CHADEMA pamoja na wajumbe wa kamati kuu ya
chama, wanaoishi kwenye Kanda ya Kaskazini pamoja na mwasisi wa chama
hicho, Edwin Mtei.
Aidha, Februari 17 mwaka huu, kikao kitajumuisha viongozi kutoka
majimbo yote ya Kanda ya Kaskazini takriban majimbo 30 na kuleta
wajumbe zaidi ya 200 katika Jiji la Arusha.
Siku hiyo hiyo kutakuwa na uzinduzi wa kanda yenyewe na
kuitambulisha timu ya uratibu, utakaohitimishwa na mkutano mkubwa wa
hadhara.
Taarifa hiyo iliwaomba wananchi, wakazi wa mikoa ya Kanda ya
Kaskazini wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya uzinduzi wa kanda yao na
kuunga mkono mpango huu wa chama ambao mbali ya kukifanya kuwa karibu
zaidi na wananchi pia katika kufanya shughuli za kisiasa kwa ufanisi wa
hali ya juu.
chanzo:mwananchi
|
|
0 comments:
Post a Comment