Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi
mkoani hapa limemkamata mtu mmoja akiwa na magunia 97 ya madawa ya kulevya aina
ya bangi ambayo yalikuwa yanasafirishwa toka mkoani hapa kuelekea Moshi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna
Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas amesema kwamba, tukio hilo lilitokea muda wa
saa 10:00 alfajiri eneo la Usa River wilayani Arumeru.
Alisema mafanikio hayo
yametokana na ushirikiano mzuri kati ya jeshi hilo na wananchi ambapo taarifa
za tukio hilo zilitolewa na raia wema ambapo askari wa jeshi hilo waliweka
mtego eneo hilo na kufanikiwa kulikamata gari aina ya Fuso lenye namba za
usajili T. 282 AAJ.
Kamanda Sabas
aliongeza kwa kusema kwamba, ndani ya bodi ya gari hilo kulikuwa na mboga aina
ya kabeji iliyosambazwa vizuri huku chini ya mboga hiyo kukiwa na madawa hayo
yaliyokuwa kwenye magunia huku yakivingirishwa kwenye mifuko ya “plastiki” kwa
ndani.
Alisema katika gari
hilo kulikuwa na watu watatu na mara baada ya askari hao kulisimamisha dereva
pamoja na msaidizi wake walifanikiwa kukimbia huku mtu mmoja aliyejulikana kwa
jina la Praygod Marick (22) Mkazi wa Dar esalaam akikamatwa.
Jeshi la polisi
Mkoani hapa linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo huku watuhumiwa wengine
wakiendelea kutafutwa. Kwa mara nyingine tena Kamanda huyo aliendelea
kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu kutokana na ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa
kwa jeshi hilo na kuendelea kuwasisitizia kuimarisha mahusiano na jeshi hilo.
Kwa muda wa kipindi cha
mwezi mmoja toka januari 07, 2013 mpaka hivi leo jeshi hilo limeshakamata
madawa ya kulevya aina ya mirungi magunia 372 katika magari mawili tofauti na
pia limeshakamata jumla ya magunia 117 ya madawa ya kulevya aina ya bangi
ambapo mwanzoni mwa wiki hii jumla ya magunia 20 yalikamatwa yakiwa
yanasafirishwa kwa kutumia wanyama aina ya Punda maeneo ya Losoiti wilayani
Longido.
0 comments:
Post a Comment