Na Rashid Nchimbi wa
jeshi la Polisi Arusha
Mtu mmoja aitwaye Joseph Loiruku Manina Mkazi wa Losinoni wilayani
Arumeru anashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani hapa baada ya kukutwa na magunia
26 ya madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo yalikuwa yanasafirishwa kwa
kutumia wanyama aina ya Punda toka eneo la Losinoni lililopo wilaya ya Arumeru kwenda
nchi jirani ya Kenya ambapo kila Punda alikuwa amebeba magunia mawili.
Hayo yameelezwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Zuberi Mwombeji alipokuwa anaongea na waandishi wa habari nje
ya jengo la Makao Makuu ya Jeshi hilo Mkoani hapa na kufafanua kwamba, tukio
hilo lilitokea juzi tarehe 11/02/2013 muda wa saa 9:30 alasiri katika eneo la Oldonyondari
lililopo Mbuga Nyeupe wilayani Longido.
Kaimu Kamanda huyo alisema kwamba, mtuhumiwa huyo akiwa na
wenzake wanne walikuwa wamepumzika katika boma mojawapo ndipo ghafla askari hao
walitokea eneo hilo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja huku wengine wanne
wakifanikiwa kukimbia. Alisema mafanikio hayo yalitokana a taarifa zilizotolewa
na raia wema toka tarehe 09/02/2013 ambazo zilifanyiwa kazi na hatimaye
kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.
Mara baada ya mahojiano ya awali, mtuhumiwa huyo alikiri
kuhusika na tukio hilo na bado jeshi hilo linaendelea na upelelezi ili kuweza
kuwakamata watuhumiwa wengine waliokimbia.
Kufuatia mafanikio hayo Kaimu kamanda huyo ameendelea
kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu kwa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo na
kuwaomba waendelee kutoa taarifa zinazohusu uhalifu na wahalifu.
Ukiachana na mafanikio
ya ukamataji wa madawa ya kulevya aina ya mirungi yaliyopatikana hivi karibuni
baada ya jeshi hilo kukamata magari mawili kwa nyakati tofauti yakiwa na viroba
374, hivi karibuni jeshi hilo limekamata magunia 117 ya madawa ya kulevya aina
ya bangi hivyo kufanya jumla ya magunia 143 yaliyokamatwa kwa muda wa mwezi
mmoja pamoja na tukio hili.
0 comments:
Post a Comment