Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa habari bangi iliyokuwa katika gunia moja kati ya magunia 20 yaliyokamatwa. |
Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jumla ya magunia 20
ya madawa ya kulevya aina ya bangi yanayokadiriwa kuwa na uzito wa kilogramu 50
kila moja yamekatwa na askari wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa. Tukio hilo
lilitokea tarehe 31/01/2013 muda wa saa 7:30 usiku katika kitongoji cha Losoiti
kijiji cha Kimokuwa wilayani Longido.
Akithibitisha
kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa
Polisi Liberatus Sabas alisema kwamba mafanikio hayo yametokana na ushirikiano
mzuri kati ya Jeshi hilo na wananchi ambapo baadhi ya raia wema walitoa taarifa
kwa jeshi hilo kuhusiana na kuwepo tukio hilo.
Kamanda Sabas
alisema kwamba, katika tukio hilo mtu mmoja mwanaume aliyejulikana kwa jina la
Mandege Pakasi (54) Mfugaji na ni mkazi wa Longido amekamatwa huku wenzake
wawili wakifanikiwa kukimbia.
Alisema kwamba watu
hao walikuwa wanasafirisha magunia hayo kutoka eneo hilo kwenda nchi jirani ya
Kenya kwa kutumia wanyama aina ya Punda ambapo jumla ya Punda 10 walitumika na
kila punda alibeba magunia mawili.
Jeshi la Polisi
Mkoani hapa bado linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo huku watuhumiwa wengine
wakiendelea kutafutwa. Kufuatia mafanikio hayo Kamanda huyo amewashukuru wakazi
wa Mkoa huu kwa ushirikiano wanaoutoa kwa jeshi hilo na ameendelea kuwaomba waendelee
kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
Ukiachana na tukio
hili kwa mwaka huu 2013 jeshi hilo mkoani hapa limekamata magari mawili yakiwa
na jumla ya viroba 374 vya madawa ya kulevya aina ya mirungi kwa nyakati
tofauti huku kesi za matukio hayo zikiwa tayari zimekwishafikishwa mahakamani.
0 comments:
Post a Comment