.

.
Wednesday, February 6, 2013

10:34 AM



Wafungwa wanaotumikia vifungo mbalimbali Mkoani Mbeya wanatembea nusu uchi kutokana na sare zao kuchakaa na kuondoa hali ya utu wa kibinadamu hali inayoonesha Wizara ya Mambo ya ndani haiwajali, licha ya Serikali kuonekana kuboresha maslahi kwa watumishi wake na kuhakikisha wanavaa sare nzuri.
Uchunguzi umebaini kuwa wafungwa katika magereza ya Ruanda, Songwe na Kawetere  ndio yaliyo katika hali mbaya na kuwafanya baadhi ya ndugu kushindwa kuwatembelea ndugu zao baada ya wafungwa hao kushindwa kujisetiri kwa adha hiyo.
Aidha mbaya zaidi ni pale wanapoamriwa kuchuchumaa chini hivyo wafungwa hao kuwa na mawazo ya namna ipi waweze kujisetiri maungo yao hasa kwa wafungwa wa jinsi ya kiume.
Katika hali ya hewa mkoani hapa ni baridi kali na wafungwa wengi hawana masweta na hivyo kubaki na sare chakavu ambazo zinahatarisha afya zao na kuwa hatarini magonjwa ya kifua na vichomi ambavyo vinaweza kusababisha vifo.
Wakuu wa magereza katika magereza hayo hawakuweza kuzungumzia lolote wakidai kuwa wao sio wasemaje wa Jeshi la magereza.
Hata hivyo juhudi za kumpata msemaji wa Jeshi la magereza makao makuu ziligonga ukuta baada ya kuambiwa kuwa msemaji yupo safarini na haijulikani siku ya kurudi kazini.  

Na, Ezekiel Kamanga Mbeya.

0 comments:

Post a Comment