.

.
Monday, February 4, 2013

2:49 PM
KWA mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2010, wabunge wa vyama vya upinzani jana waliungana pamoja na kumsusia Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, wakipinga hatua yake ya kupindisha hoja binafsi ya Mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na kuitetea serikali bila maelezo yanayoeleweka.
Kwa pamoja, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), National Convention for Construction and Reform (NCCR- Mageuzi), United Democratic Party (UDP) na Chama cha Wananchi (CUF) walitoka nje ya ukumbi wa Bunge wakaenda ukumbi wa kambi ya upinzani kufanya kikao cha dharura juu ya hatua za kuchukua dhidi ya ubabe wa Ndugai.
Hatua kama hiyo ya kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, imekuwa ikitumiwa na wabunge wa CHADEMA ambayo inaunda kambi rasmi ya upinzani bungeni kupinga baadhi ya masuala kadhaa.
Hata hivyo, kwa mara mbili tofauti CHADEMA waliposusia Bunge, wenzao wa vyama vingine hawakuwaunga mkono, hatua iliyotafsiriwa kama kutokuwapo kwa mshikamano.
Kwa mara ya kwanza, CHADEMA walisusia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kufungua Bunge, wakipinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliyomleta madarakani na mara ya pili walitoka nje ya ukumbi wakipinga kupitishwa kwa sheria ya mabadiliko ya katiba mpya.
Hali hiyo ni tofauti na jana ambapo wabunge wa vyama hivyo vya CHADEMA, CUF, UDP, TLP na NCCR-Mageuzi waliungana kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, kupinga hatua ya Ndugai kuwaburuza katika kupitisha hoja ya Mbatia.
Hoja hiyo binafsi iliyoainisha udhaifu katika mfumo wa elimu nchini, iliwasilishwa juzi na kuibua mjadala mzito bungeni, huku kambi ya upinzani ikikubali hoja ya Mbatia kutaka kuunda kamati teule wakati wabunge wa CCM wakipinga.
Mzozo wa jana ulianza baada ya Mbatia kufunga hoja yake na kutaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ampe nakala ya mitaala ya elimu aliyoionesha bungeni kwamba anayo.
Mbatia alitaka kupata nakala hiyo ya mitaala akidai Tanzania haijawahi kuwa na mitaala ya elimu tangu mwaka 1961, huku Waziri Kawambwa akidai anayo.
Baada ya Kawambwa kushindwa kukabidhi nakala ya mitaala hiyo kwa Mbatia, mbunge huyo aliacha kuendelea kufunga hoja yake, akasema waziri amelidanganya Bunge.
Tangu Bunge lililopita serikali ilikuwa imeombwa, na nayo ikaahidi kuleta mitaala hiyo bungeni. Mbatia alishauri serikali iwagawie wabunge nakala ya mitaala hiyo.
Kwa sababu anazojua mwenyewe, Ndugai, badala ya kuitaka serikali itekeleze ahadi yake, akaitetea kijanja, akimtaka Mbatia ahitimishe hoja yake kwanza, kwa madai kuwa mwenyewe angetafuta namna ya kuieleza serikali ilete mitaala hiyo baadaye.
Ndipo Mbatia alipoomba mwongozo wa spika, na Ndugai akagoma kuruhusu mwongozo utolewe, huku akimsuta mbunge huyo, kama vile anamlazimisha, kwamba muda huo anaotumia kuomba mwongozo ndio muda wake kuhitimisha hoja yake binafsi.
Mbatia akasema haikuwa mara yake ya kwanza kuomba mitaala hiyo, kwani hata jana yake alikuwa amemwandikia waziri wa elimu kuomba mitaala hiyo; na kwamba alishafika hata wizarani akanyimwa nakala ya mitaala. Akahoji iweje mbunge adanganywe hivyo, tena katika suala nyeti kama hili?
Wakati Mbatia akiendelea kushikilia msimamo wake, wabunge kadhaa wa CHADEMA na NCCR-Mageuzi nao wakaingilia kati kuomba mwongozo wa spika, lakini Ndugai akawagomea, akisema yeye ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuomba nakala ya mitaala serikalini.
Baada ya kibano cha wapinzani, Ndugai akatumia ubabe kuhitimisha hoja ya Mbatia, akamwita Mbunge wa Nzega, Hamis Kigwangalla awasilishe hoja yake.
Kutokana na ubabe huo, wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya ukumbi wa Bunge na kufanya mkutano na waandishi wa habari.
Wakizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Pius Msekwa, kambi hiyo ya upinzani ilimtaka Waziri Kawambwa kujiuzulu kwa sababu amelidanganya Bunge kwamba anayo mitaala ya elimu wakati hana.
Mbali ya hayo, walimwomba Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua hesabu za Wizara ya Elimu hususani katika miradi ya uchapishaji vitabu.
Pia walisema watatumia kanuni ya 14 ya Bunge kuandaa hoja ya kuwaondoa madarakani, Spika Anne Makinda na Naibu wake, Ndugai kwa sababu wameshindwa kuendesha Bunge hilo kwa haki bila upendeleo.
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu (CHADEMA), alisema katika Bunge lililopita Dk. Kawambwa aliahidi kuleta hadharani mitaala ya elimu ya shule za msingi na sekondari, lakini hakufanya hivyo.
Alisema kwa mara ya pili jana, wakati akijibu hoja za Mbunge wa kuteuliwa, Mbatia aliahidi kuileta, lakini hakufanya hivyo.
“Kama mnakumbuka, jana mheshimiwa Mbatia alisema yuko tayari kujiuzulu kama waziri angeweza kuleta hiyo mitaala, lakini waziri alizidi kusisitiza kwamba mitaala ipo wakati si kweli, pia kibaya zaidi waziri alisimama na kuonyesha kwamba alikuwa na mitaala hiyo mkononi kumbe kile alichokuwa akikionyesha ni muhtasari na si mtaala.
“Hii ina maana kwamba, alichokionyesha waziri hiyo si mitaala bali rasimu ya mwaka 2005, kwa maana hiyo ni wazi Waziri Kawambwa amelidanganya Bunge,” alisema.
Lissu alisema wapinzani kuanzia sasa wanaanza kuandaa taarifa kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo kumtaka Waziri Kawambwa kujiuzulu na asipofanya hivyo, wataiomba mamlaka ya uteuzi imfukuze kazi.
Aliongeza kuwa yasipofanyika hayo yote, watapeleka hoja bungeni ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Aidha, katika mkutano huo, wapinzani hao walidai kuwa Spika Makinda pamoja na naibu wake, Ndugai wanaongoza Bunge hilo kibabe na kuwazuia wabunge kuisimamia serikali sawasawa.
“Spika na naibu wake, wamefanya kila jitihada kuikinga serikali na kulizuia Bunge kuisimamia na kuiwajibisha serikali kuhusu uchafu huu wa mitaala kwa shule zetu.
“Sisi wabunge wa upinzani pia tumeazimia kuandaa hoja bungeni ya kuwaondoa Spika wa Bunge na naibu wake madarakani,” alisema Lissu.
Aidha, Lissu alisema watatumia fursa zilizopo ili kuhakikisha mjadala wa mitaala kwa shule za Tanzania unapata nafasi ya kujadiliwa na Bunge kwa uwazi na kwa haki.
Naye Mbatia alisema ameshangazwa na hoja yake kutoungwa mkono na wabunge wa CCM kwa sababu Tanzania haijawahi kuwa na mitaala tangu mwaka 1961.
“Naibu Spika alipata kigugumizi gani kunipa hiyo mitaala ili niweze kujiridhisha na pengine kuondoa hoja yangu ili kuweka sawa hansadi za Bunge?
“Nasema suala hili hatutaliacha hadi watueleze fedha zilizotolewa na taasisi za kigeni kugharamia vitabu vya watoto wetu zilifanya kazi ipi, wanafichaficha ili pia watumie fedha (chenji) za rada kutengeneza tena uchafu huo wa vitabu,” alisema Mbatia.
chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment