.

.
Monday, February 4, 2013

1:45 PM
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa habari bangi iliyokuwa katika gunia moja kati ya magunia 20 yaliyokamatwa.
  
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jumla ya magunia 20 ya madawa ya kulevya aina ya bangi yanayokadiriwa kuwa na uzito wa kilogramu 50 kila moja yamekatwa na askari wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa. Tukio hilo lilitokea tarehe 31/01/2013 muda wa saa 7:30 usiku katika kitongoji cha Losoiti kijiji cha Kimokuwa wilayani Longido.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas alisema kwamba mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Jeshi hilo na wananchi ambapo baadhi ya raia wema walitoa taarifa kwa jeshi hilo kuhusiana na kuwepo tukio hilo.
Kamanda Sabas alisema kwamba, katika tukio hilo mtu mmoja mwanaume aliyejulikana kwa jina la Mandege Pakasi (54) Mfugaji na ni mkazi wa Longido amekamatwa huku wenzake wawili wakifanikiwa kukimbia.
Alisema kwamba watu hao walikuwa wanasafirisha magunia hayo kutoka eneo hilo kwenda nchi jirani ya Kenya kwa kutumia wanyama aina ya Punda ambapo jumla ya Punda 10 walitumika na kila punda alibeba magunia mawili.
Jeshi la Polisi Mkoani hapa bado linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo huku watuhumiwa wengine wakiendelea kutafutwa. Kufuatia mafanikio hayo Kamanda huyo amewashukuru wakazi wa Mkoa huu kwa ushirikiano wanaoutoa kwa jeshi hilo na ameendelea kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
Ukiachana na tukio hili kwa mwaka huu 2013 jeshi hilo mkoani hapa limekamata magari mawili yakiwa na jumla ya viroba 374 vya madawa ya kulevya aina ya mirungi kwa nyakati tofauti huku kesi za matukio hayo zikiwa tayari zimekwishafikishwa mahakamani.

0 comments:

Post a Comment