.

.
Wednesday, February 13, 2013

11:51 AM
Na Rashid Nchimbi wa jeshi la Polisi Arusha
Mtu mmoja aitwaye Joseph Loiruku Manina Mkazi wa Losinoni wilayani Arumeru anashikiliwa na jeshi la Polisi Mkoani hapa baada ya kukutwa na magunia 26 ya madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo yalikuwa yanasafirishwa kwa kutumia wanyama aina ya Punda toka eneo la Losinoni lililopo wilaya ya Arumeru kwenda nchi jirani ya Kenya ambapo kila Punda alikuwa amebeba magunia mawili.

Hayo yameelezwa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Zuberi Mwombeji  alipokuwa anaongea na waandishi wa habari nje ya jengo la Makao Makuu ya Jeshi hilo Mkoani hapa na kufafanua kwamba, tukio hilo lilitokea juzi tarehe 11/02/2013 muda wa saa 9:30 alasiri katika eneo la Oldonyondari lililopo Mbuga Nyeupe wilayani Longido.

Kaimu Kamanda huyo alisema kwamba, mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake wanne walikuwa wamepumzika katika boma mojawapo ndipo ghafla askari hao walitokea eneo hilo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja huku wengine wanne wakifanikiwa kukimbia. Alisema mafanikio hayo yalitokana a taarifa zilizotolewa na raia wema toka tarehe 09/02/2013 ambazo zilifanyiwa kazi na hatimaye kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo.

Mara baada ya mahojiano ya awali, mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na tukio hilo na bado jeshi hilo linaendelea na upelelezi ili kuweza kuwakamata watuhumiwa wengine waliokimbia.

Kufuatia mafanikio hayo Kaimu kamanda huyo ameendelea kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu kwa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo na kuwaomba waendelee kutoa taarifa zinazohusu uhalifu na wahalifu.

Ukiachana na  mafanikio ya ukamataji wa madawa ya kulevya aina ya mirungi yaliyopatikana hivi karibuni baada ya jeshi hilo kukamata magari mawili kwa nyakati tofauti yakiwa na viroba 374, hivi karibuni jeshi hilo limekamata magunia 117 ya madawa ya kulevya aina ya bangi hivyo kufanya jumla ya magunia 143 yaliyokamatwa kwa muda wa mwezi mmoja pamoja na tukio hili.

0 comments:

Post a Comment