.

.
Monday, November 18, 2013

Na, Bertha Ismail-Kiteto

CHAMA cha Wakulima na Wafugaji wilayani Kiteto mkoani Manyara(CHAWAKI) kimeibua shutuma dhidi ya viongozi wa CCM wilaya na mkoa wa Kiteto Mkoani Manyara.

Aidha pia Baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho tawala limelezwa kuwa chanzo cha mgogoro katika eneo linalodaiwa kuwa la hifadhi ya Jamii ya Emborley Murtangos kwa kujenga mfumo wa matabaka yanayosababisha kuwepo kwa mapigano kati ya jamii ya wakulima dhidi ya wafugaji.

Mfumo huo wa matabaka umedaiwa kuongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoani hapa Lucas Kasmir Ole Mukus kwa kudaiwa kuchangisha  fedha kwa wafugaji  kwa ajili ya kukusanya kiasi cha shilingi 150,000,000/= ili kuwezesha kuendesha operesheni ya kuwaondoa wakulima na kuwaacha wafugaji katika eneo hilo hali iliyoleta mtafaruku baina ya viongozi hao, wafugaji na wakulima.

Hata hivyo ili kuthibitisha hivyo, CHAWAKI  kinaeleza kuwa katika operesheni iliyobarikiwa na viongozi hao kupitia vikao vya kimila vinavyopigiwa chapuo na mwenyekiti wa CCM mkoa kwa  kuhamasisha  wafugaji ambao wengi wao ni wamasai kuchanga ngombe kwa madai ya kuwatoa wakulima kwa kuwaita wavamizi  ili kuwabakiza wafugaji pekee katika hifadhi hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara  wa kufunga ziara yake, mjumbe wa halmashauri kuu-Taifa(M-NEC) Emmanuel John Papian uliofanyika kwenye kijiji cha Engusero mbele ya ,mwenyekiti wa CHAWAKI Hassani Loosiok anaeleza kuwa mfumo huo wa matabaka ya ukabila unaojengwa na viongozi hao endapo hautadhibitiwa eneo hilo halitakuwa na amani kamwe.

“Hii ishu ya hifadhi imeshakuwa hot cake...Tatizo linaloonekana hapa kwanza kuna tatizo la tafsiri ya hukumu ya hifadhi ya emborley murtangos,hukumu ilielekeza haimhitaji mkulima ama mfugaji kufanya shughuli zake katika eneo hilo la hifadhi,lakini  nimebaini kuwa hakuna mkutano mikuu ya vijiji saba vilivyofanya uamuzi wa kupatikana kwa hifadhi ya emborley murtangs kama inavyotajwa hali inayoonyesha kuwa viongozi wanaochochea mgogoro huo wana maslahi na hifadhi hiyo bubu” alisema Losiok.

Aliwataka viongozi kuchukua jukumu la kuhakikisha kuwa wanadumisha uhusiano mzuri kati ya pande zote mbili kutokana na ukweli kuwa hali hiyo ya jamii ya wafugaji imekuwa ikitumika kupitia mikutano ya kimila inayohudhuriwa na viongozi hao kuchangisha fedha za kuondolewa kwa wakulima  kitendo ambacho kitaendelea kusababisha machafuko makubwa kwa kuwa tabaka la wafugaji limekuwa likibebwa na viongozi hao na hii inatokana na kuwa wengi wa viongozi hao ni wamasai ambao nao ni wafugaji na wana ngombe wanaolishwa  katika hifadhi hiyo.

“Hali hii inajenga taswira ya chuki baina ya wakulima na wafugaji…,nimesoma barua ya mkurugenzi kwa niaba ya RC inayowataka wenyeviti, watendaji vijiji,kata na tarafa ya kuwaondoa wafugaji na wakulima lakini hawa jamaa wanawatoa wakulima pekee hali itakayo sababisha vita baina ya wakuma na wafugaji ambapo mbeleni wafugaji wataleta fujo isiyoisha baina yao na serikali kwa kuchukua fedha zao kwa kuwalaghai.

Alisema kulingana na taswira ya eneo hilo kwa kipindi chote hicho cha mgogoro huo halmashauri licha ya kuwaondoa wakulima kwa kuvunja makazi yao, tangu mwaka 2002, eneo hilo halikuwa  limesajiliwa kama hifadhi bali ndio limesajiliwa  Oktoba 25 mwaka huu chini ya wizara ya Mambo ya ndani kitengo cha usajili wa vyama vya siasa badala ya wizara ya maliasili na utalii, huku CHAWAKI wakisajili Oktoba 7 kupitia wizara ya Mali Asili na Utalii.

Msemaji wa CHAWAKI Hassan Loosiok alisema mbele ya M-NEC huyo kuwa baraza la Madiwani la halmashauri hiyo limekuwa likishiriki kupotosha pamoja na kupuuza maamuzi ya wananchi wa vijiji kwani eneo hilo lilitengwa na wananchi wa vijiji saba kama eneo la hifadhi ya jamii na sio hifadhi ya Emborley  Murtangos huku vijiji vitano  vikiendesha mikutano mikuu na kuamua kujitoa kwenye mpango wa hifadhi wa Emborley murtangos.

“Sasa sisi tunasema sehemu ya kushtakia ni hapa CCM ambacho ndicho chama wanachokitumikia kuwa ifikie mahali muwaambie waheshimiwa madiwani waheshimu maamuzi ya wananchi wasifanye mambo kwa matakwa binafsi..,M-nec tunao ushahidi wa vijiji vitano kujitoa kwenye mpango wa  hifadhi hiyo na hili litakuthibitishia kuwa CCM haina madiwani watetezi wa wananchi bali ni madiwani wanaotetea maslahi yao binafsi.

Alivitaja vijiji vilivyojitoa kwenye mpango huu kuwa ni Nati,Emarit,Engusero-Sidani,Kimana na Lotepes,huku vijiji vya Namelok na Ndiligishi vikiwa bado havijafanya mikutano mikuu ya vijiji.

Hata hivyo  kulingana na halmashauri kusajili eneo hilo kupitia kitengo cha vyama ya siasa Loosiok alisisitiza kuwa ,madiwani hao hawana mamlaka ya kumiliki ardhi ama mamlaka ya kutumia dola  kuwaondoa wakulima na wafugaji kwa mujibu wa sheria Na 5/1999 kwa kuwa ardhi hiyo ni mali ya kijiji na sio mali ya halmashauri ya wilaya hiyo.

Mbali na hali hiyo  alikwenda mbali kwa kumtupia lawama mwenyekiti wa CCM mkoani hapa Lucas Ole Mukus kwa kumtuhumu  kuendesha vikao vya mila vyenye lengo la kukusanya fedha hizo ,huku na baadhi vikimshirikisha mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo bi Jane Mutagurwa aliyeandika barua  Kumb:Na,HMW/KT/E/09/VOL II/13 ya Novembe 5,2012 kwa wenyekiti wa Mila wa vijiji 31 kuchangisha fedha za kuwaondoa wavamizi.

Akipokea malalamiko hayo mjumbe wa halmashauri kuu Emmanuel John Papian alisema kulingana na mwenendo mzima wa mgogoro huo amebaini baada ya kutembelea kata zote za halmashauri ya wilaya hiyo kuwa mgogoro huo umengiliwa na ukabila,siasa za viongozi ambao hawaweze kutoa Haki na Usawa kwa kuwa baadhi yao ni wadau.

Kulingana na ugumu wa kufikia muafaka wa mgogoro huo,Papian alisisitiza kuwa CCM itakachofanya ni kuhakikisha wanataraji kupeleka ombi hilo kwa waziri Mkuu Mizengo Kayanza Pinda kutatua mgogoro huo kwa kuwa hakuna njia nyingine ya kufikia muafaka ispokuwa yeye tu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mainge Lemalali alikiri kuendeshwa kwa zoezi hilo la ukusanyaji wa fedha ambap alisema lililenga kujenga shule na pia fedha nyingine zikielekezwa kulipia deni la kesi walizonazo juu ya hifadhi hiyo juu ya kuwatoa wakulima ,huku mwenyekiti wa CCM mkoani hapa Lucas Ole Mukus akieleza vikao vya kimila vililenga kuhimiza kuchangia mfuko wa elimu na kutaka kuwapuuza wanaomshtumu.
MWISHO


0 comments:

Post a Comment