Na Bertha
Ismail –Hanang.
Baada ya
kukamilika kwa miundombinu ya
barabara kwa kiwango cha lami,
kutoka Minjingu-Babati hadi Singida Mkoani Manyara hatimaye serikali ya mkoa
huo iko mbioni kuanza ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kisasa kinachotarajiwa kuanza
kujengwa wilayani Babati.
Kwa mujibu
wa mkuu wa Mkoa huo, Elaston John Mbwillo, kwa sasa serikali mkoani humo
imeomba wataalam kutoka wizarani kuja kukagua maeneo yaliyopendekezwa ya
Endakiso na Magugu ili kujua hali ya mazingira ya uelekeo wa upepo.
Mbwillo
ametaja baadhi ya malengo ya kujengwa kwa uwanja huo kuwa ni kupunguza gharama za kuwapokea wageni
pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo wa serikali wanaokuja mkoani humo na pia
kutoa fursa kwa wawekezaji kuweza kuwekeza.
“Malengo
makubwa ya kutaka kujenga uwanja wa ndege hapa mkoani kwetu ni pamoja na
kupunguza gharama za kwenda kuwapokea wageni wetu wakiwemo viongozi wa serikali
kwani tumekuwa tukilazimika kwenda hadi Arusha kuwapokea viongozi wanaotaka
kufika kwetu hali ambayo imekuwa ikitulazimu kujaza magari yetu mafuta ya
kutembea umbali wa kilometa zaidi ya 150 kwa gari moja,”Alisema mkuu huyo na
kuongeza,
“Na kama
unavyojua mapokezi ya kiongozi wa serikali huwezi kufanya mwenyewe lazima uwe
na maafisa usalama na baadhi ya wakuu wa idara…si unaona ilivyo ghamara kubwa,
matokeo yake tutakuwa tunatumia rasilimali nyingi kwa kitu kimoja”.Alisema
Mbwilo.
Alisema kuwa
mbali na gharama pia wanakuwa hawana
uhakika na usalama wa wageni wao kwani maafisa usalama wanaowapokea si mkoa wake
pia wananchi wanaopishana nao hawafahamiani sambamba na baadhi ya maeneo
wanayopitishwa.
Mbwilo
aliongeza kuwa mbali hayo pia mkoa wa Manyara ukimiliki uwanja wake wa ndege
utasaidia kulinda uchumi wa mkoa ikiwemo biashara kuwepo.
Kwa mujibu
wa taarifa ya miundo mbinu ya mtandao wa barabara mkoani humo,kwasasa
umefanikiwa kuwa na mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami wenye
urefu wa km 203.7 kati ya mtandao wenye km 6,010.
Aidha baadhi
ya wakazi wilayani Babati Ali Hamza mkazi wa mji mdogo wa Magugu amesema
taarifa ya ujenzi huo ilianza kuzungumzwa kwenye majukwaa ya siasa na vikao
mbalimbali kwa takribani miaka 10 sasa,lakini endapo ujenzi huo utafanyika basi
utasaidia kupanda kwa uchumi wa mkoa huo na wananchi wake.
Hata hivyo
licha ya kuwepo kwa mkakati wa kujengwa kwa uwanja huo,kwasasa mkoa huo una
vituo vidogo vya ndege 49 (airstrips) katika maeneo ya wilaya zote tano
vinavyoruhusu kutua kwa ndege ndogo kwa ajili ya kusaidia kusafirisha watalii.
Fursa
nyingine ni kusafirisha wagonjwa waliopata rufaa na flying doctors wanaotumika
kuokoa maisha ya majeruhi kabla ya kufikishwa hospitalini.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment