.

.
Wednesday, November 13, 2013


 
DK SENGONDO MVUNGI.

DAR ES SALAAM. 
MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi (61) amefariki dunia katika Hospitali ya Millpark Netcare, Johanesburg, Afrika Kusini.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana kutoka Afrika Kusini na kuthibitishwa na Msemaji wa Hospitali ya Millpark, Tebogo Nyembezi zinasema Dk Mvungi alifariki dunia jana mchana. “Ni kweli tulimpokea mgonjwa huyo kutoka Tanzania na alifariki 6:00 mchana (saa 7:00 kwa saa za Afrika Mashariki),”alisema Nyembezi.
Nyembezi alisema kwamba walimpokea mgonjwa huyo akiwa na majeraha ya kichwa, lakini aliahidi kueleza sababu ya kifo chake leo baada ya kuzungumza na madaktari waliokuwa wakimtibu.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba pia alithibitisha kupokea taarifa za kifo hicho na kwamba walikuwa wakiendelea kuandaa taratibu za kuleta mwili wake nchini.
“Ni pigo kubwa kwetu, tunaangalia namna ya kuusafirisha kuja nchini na baadaye tutatoa taarifa rasmi,”alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Kwa kweli ni pigo kubwa siyo kwetu tu, lakini pigo kubwa kwa nchi yetu, tumepoteza mtu muhimu na kiungo muhimu sana. Dk Mvungi, wengine tulimfahamu tangu alipokuwa mwanafunzi, alikuwa mtu aliyesema kile alichokiamini, akikwambia kitu kilikuwa ni kile kilichopo moyoni mwake”.
Jaji Warioba alisema Dk Mvungi alikuwa msomi aliyebobea katika masuala ya sheria na kwamba alikuwa na mchango mkubwa katika tume. Pia alisema marehemu atakumbukwa kwa ushiriki wake wa dhati katika kupigania haki za binadamu, kazi aliyoifanya kwa moyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani alisema: “Dk Mvungi alikuwa mfanyakazi hodari, alikuwa hachoki na hata ulipotokea ubishi mkubwa katika majadiliano kiasi cha watu wengine ku-loose temper (kupandwa na jazba), yeye alibaki vilevile na alizungumza vilevile bila kubadilika. 


Kweli tumempoteza mtu muhimu sana maana alikuwa akifahamu vizuri sana sheria, hatuna jinsi maana tumempoteza, kwahiyo itabidi tuendelee na kazi hii. Hatuna namna nyingine ya kufanya,”alisema Jaji Ramadhani.
Jaji Ramadhani alisema taratibu nyingine zitatangazwa baadaye kwani lazima washirikiane na chama chake, NCCR- Mageuzi alikokuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, familia yake na Chuo Kikuu cha Bagamoyo ambako alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia aliliambia gazeti hili kwamba walipokea taarifa ya kifo cha Dk Mvungi saa 9.30 alasiri jana. “Tumepokea taarifa hizo alasiri kwamba amefariki. Ni kweli na sasa ninaelekea nyumbani kwake ili kuitaarifu familia,”alisema Mbatia.
Taarifa ya Tume
Jana jioni, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa taarifa rasmi kuhusu kifo cha Dk Mvungi ikisema: “Kwa masikitiko makubwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi kuwa Mjumbe wake Dk Sengondo Mvungi aliyekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Millpark iliyopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini amefariki dunia.”.

 MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment