.

.
Monday, November 18, 2013

9:45 PM

Magari ya kubebea wagonjwa yalionekana eneo la Uwanja wa Ndege jijini Kazn, Urusi. 

Ndege ya abiria imeanguka katika uwanja wa ndege katika mji wa Kazan, nchini Urusi na kuua watu wote 50 waliokuwa katika ndege hiyo.Ndege hiyo aina ya Boeing 737 iliruka kutoka mji wa Moscow na ilikuwa ikijaribu kutua lakini ikawaka moto saa moja usiku kwa saa za huko.

Wizara ya matukio ya dharura imesema kulikuwa na abiria 44 na wafanyakazi sita wa ndege hiyo ya shirika la Tatarstan Airlines.

Afisa wa kamati ya uchunguzi Vladimir Markin ameiambia Televisheni moja nchini Urusi, Rossiya 24 TV, kwamba wataalam wanachunguza kubaini kama ajali hiyo imesababishwa na matumizi ya mafuta mabaya, au hali mbaya ya hewa.Wachunguzi wanajaribu kuona kama kulikuwa na makosa ya kiufundi au huenda ya kibinadamu yaliyosababisha ajali hiyo.
Mvua ilikuwa ikinyesha katika mji wa Kazan wakati ndege hiyo ilipoanguka.
Kwa mujibu wa orodha rasmi ya wasafiri wa ndege hiyo, miongoni mwa waliokufa ni Irek Minnikhanov, mtoto wa kiume wa rais wa Jamhuri ya Tatarstan,nchini Urusi.
Aleksander Antonov, ambaye aliongoza Idara ya Usalama ya Shirikisho la Urusi, ni miongoni mwa abairia wa ndege iliyoanguka.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza, imethibitisha kuwa raia mmoja wa Uingereza amekufa katika ajali hiyo.
Miongoni mwa waliokufa wamo watoto wawili.
Rais Vladimir Putin wa Urusi ametuma salaama zake za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa waathirika.
Tume ya serikali imeundwa kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
Taarifa zinasema, rubani wa ndege hiyo Rustem Salikhov mwenye umri wa miaka 47, alijaribu mara kadhaa kutua kabla ya kuanguka kwa ndege hiyo.
Shirika la habari la Urusi limeripoti kuwa wafanyakazi walisema hawakuwa tayari kutua kwa sababu ya matatizo ya kiufundi.
Mwandishi mmoja wa habari ambaye alisafiria ndege hiyo mapema Jumapili kabla ya safari iliyotokea ajali, kutoka Kazan kwenda Moscow ameiambia televisheni moja nchini Urusi kwamba kulikuwa na mtetemo mkubwa wakati ndege hiyo ikitua mjini Moscow.
"Tulipokuwa tukitua haikujulikana kama kulikuwa na upepo mkali, japokuwa mjini Moscow, hali ya hewa ilikuwa nzuri au kulikuwa na tatizo la kiufundi au ndege yenyewe," amesema Lenara Kashafutdinova.
"Tulisukwasukwa huku na kule, ndege ilitua. Mtu aliyekuwa amekaa karibu nami alikuwa mweupe kama shuka kutokana woga uliompata."
Ndege hiyo imekuwa ikitoa huduma tangu mwaka 1990.
Uwanja wa ndege wa Kazan - mji mkuu wa Tatarstan - umefungwa tangu kutokea jali hiyo na hautarajiwi kufunguliwa hadi Jumatatu mchana.
Mji wa Kazan upo kilomita 720 mashariki mwa Moscow.

0 comments:

Post a Comment