.

.
Wednesday, November 13, 2013

2:05 AM


 

 

Mfanyabiashara wa Madini ya Tanzanite,Vailet Matias (37), Mkazi wa Njiro Arusha aliyepigwa risasi na polisi Oktoba 31 mwaka huu mkoani Arusha, amehamishiwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Center inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Mfanyabiashara huyo alipigwa risasi baada ya kudaiwa kutaka kumpiga risasi polisi aliyekuwa lindoni, akitumia bastola yake kutokana na malumbano ya maegesho ya magari. Awali alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, akiwa chini ya uangalizi mkali.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Paulo Kisanga alisema jana kuwa Vailet alihamishiwa chumba cha wagonjwa mahututi tangu juzi kutokana na hali yake kuwa mbaya kutokana na jeraha.
“Ni kweli huyu mgonjwa yupo ICU, mimi nipo nje ya hospitali ila kabla ya kuondoka nilimwacha akiwa katika chumba hicho akipatiwa matibabu” alisema Dk Kisanga.
Taarifa ya Dk Kisanga ilitolewa wakati kukiwa na uvumi wa kufariki kwa mfanyabiashara huyo, ambao jana ulisambaa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana kuwa alikuwa hana taarifa kamili za afya ya mgonjwa huyo.
Alisema awali baada ya mfanyabiashara kuegesha gari hilo mbele ya lango kuu la kuingia katika Tawi la Benki ya CRDB, alitakiwa kulitoa na akagoma ndipo polisi walilitoa upepo na kwamba alipokuta limetolewa upepo ndipo alipoanza kulumbana na polisi hadi akapigwa risasi.

0 comments:

Post a Comment