.

.
Friday, March 14, 2014

3:51 AM
Na Lorietha Laurence-Maelezo

Asilimia 1.03 ya vifo hutokana na ugonjwa wa figo, hayo yalisemwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii  Seif Rashidi alipokuwa akitoa tamko kwa waandishi wa habari  leo jijini Dar es salaam,kuhusu siku ya afya ya figo itakayoadhimishwa  tarehe 13 Machi,mwaka huu mjini Dodoma.

 Kauli mbiu ya maadhimisho hayo “Figo huzeeka, kadiri mtu anavyozeeka. Jali Afya ya Figo zako”. Lengo ni  kuelimisha  jamii ili iweze kuelewa umuhimu wa  figo katika   mwili, watu kubadili staili za maisha, kuhamasisha  watoa huduma kuhusu wajibu wao katika kugundua magonjwa ya figo na kupunguza hali hatarishi za ugonjwa sugu wa figo na kuandaa mikakati madhubuti ya kukinga na kuthibiti magonjwa ya figo.

“ Nawasihi watu wawe na taratibu za kufanya vipimo mara kwa mara, pia kujali afya zao kwa kuwekeza katika maendeleo ya afya zao ili kujikinga na ugonjwa wa figo” alisema Mhe.Rashidi .

Aliongeza kuwa ugonjwa huo husababishwa na shinikizo la damu,ugonjwa wa kisukari na kutokufanya mazoezi mara kwa mara,msongo wa mawazo,unywaji  pombe, unene uliokidhiri,ulaji usiofaa , matumizi ya chumvi na mafuta pamoja na uvutaji sigara.

Alifafanua kuwa ugonjwa  huo unaweza  kumuathiri mtu yeyote aliye katika umri wowote, ingawa hujitokeza zaidi kwa watu wenye umri wa miaka 50, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwanaume mmoja kati ya watano  na mwanamke mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 65 hadi 74 wana ugonjwa wa figo.

Pia alieleza kwamba figo ni kiungo muhimu  katika mwili wa binadamu, husaidia  katika kuchuja na kuondoa taka mwilini ,majimaji  yaliyozidi na kudhibiti kiwango cha kemikali mwilini kwa kudhibiti shinikizo la damu.

Aliwataka  watu waepukane na ugonjwa huu wa figo, kwa kufuata ushauri wa wataalama na  kuzingatia mazoezi, kunywa  glasi 6 hadi 8 za maji kwa siku,kuepuka matumizi ya sigara na bidhaa zinazotokana na tumbaku, kuzingatia maelekezo ya wataalam, kutumia dawa kwa usahihi na kufuatilia kiwango cha sukari mwilini.
  .

Maadhimisho ya afya ya figo duniani yalianza mwaka 2006,ambapo mwaka huu yataadhimishwa kuanzia tarehe 10 hadi 14 Machi, katika viwanja vya Mwalimu Nyerere mjini Dodoma,shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kutoa huduma ya kupima afya ya figo,kutoa ushauri nasaha na kutoa tiba na rufaa.

0 comments:

Post a Comment