.

.
Friday, March 14, 2014


MWANAMKE mmoja mkazi wa Kimandolu jijini Arusha, Suzy Mrema (40) anayeishi na virusi vya Ukimwi amedai kutengwa na ndugu zake, ikiwa ni pamoja na kunyimwa urithi wa mali za marehemu baba yao kwa madai ya kuwa yeye ni marehemu mtarajiwa.
Akizungumza na gazeti hili, Suzy, mtoto wa kwanza kuzaliwa kwa marehemu Mzee Thomas Mrema aliyeacha wake watatu, watoto 21 na mali zikiwemo nyumba kadhaa, amekiri kuishi na virusi vya Ukimwi kwa muda mrefu.
Alisema kwamba anasikitishwa na kitendo cha wadogo zake kumtenga na kugoma kumgawia sehemu ya mali za marehemu baba yake, kwani tangu afariki dunia miaka 10 iliyopita ndugu zake hao wamemtimua nyumbani, wakidai hana faida yoyote katika familia yao na muda wowote anaweza kufa kutokana na maradhi yanayomsibu.
“Kaka yangu, mimi ni mwathirika wa Ukimwi na hata dawa ninazotumia hizi hapa (anaonesha makopo matatu) ila hawa wadogo zangu wamekuwa wakininyanyapaa kwa muda mrefu na kuniita marehemu mtarajiwa,” alisema na kuongeza;
“Hivi sasa unavyoniona sina kazi maalumu ya kufanya nimekuwa nikibangaiza kwa kuuza mboga na kufua nguo za watu majumbani ambao hunilipa ujira kidogo, baba yangu ameacha mali nyingi sana ila wamejigawia wenyewe na kunitenga mimi kwa kuwa ni mwathirika.”
Alisema baba yake kabla ya kufariki alikuwa anaishi na wake watatu, akiwemo mama yake mzazi ambaye yupo hai, alisema upande wa mama yake walizaliwa watoto 10 na watoto watatu walifariki dunia na kubakia saba.
Alisema wake wawili wa baba yake pia walifariki dunia na kuacha jumla ya watoto 14 na kati yao watoto wanne walifariki na kubaki 10 ambao hadi sasa bado wapo hai, huku watoto wa kiume wakikataa kumgawia mali hizo na kukataa hata kuuzwa kwa mali hizo ili wagawane fedha.
Alisisitiza kuwa licha ya kulifikisha suala hilo katika ngazi mbalimbali, ikiwemo ofisi ya mtendaji wa kata, kituo cha sheria na haki za binadamu na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Raymond Mushi ambaye kwa sasa amehamishiwa Dar es Salaam, hakupata ufumbuzi wa suala hilo.
Mwanamke huyo ameiomba serikali, taasisi mbalimbali na mashirika yanayojihusisha na haki ya mwanamke na mtoto, kumsaidia ili aweze kupata haki yake.
Kwa upande wa mama yake mzazi, Rose Thomas Mrema alikiri kunyanyapaliwa kwa mwanawe huyo na kusisitiza kuwa watoto wake wa kiume wakiwemo wa wake wengine ndio wanashiriki kutumia ubabe kudhulumu wenzao na kujigawia mali hizo wenyewe.
Alipoulizwa kaka mkubwa wa Suzy, Severine Mrema alikiri wanandugu kutompa mgawo dada yao, huku akisisitiza kuwa, kigezo si ugonjwa wake, bali ni kwa sababu ameshaolewa na anaendesha maisha yake akiwa nje ya familia hiyo.
Kaka huyo wa pili kuzaliwa katika familia ya Mrema, akizungumza kwa njia ya simu kutoka Tanga anakoishi na kufanya biashara, alisema; “Kwa mila za kiafrika, hawezi kupata mgawo wa mali kwa sababu ana mji wake.
Na si yeye pekee, wako wengine kama watano, lakini kwa kuwa amekwenda kudai haki katika vyombo vya sheria, tusubiri. Kama akifanikiwa atakuwa amewasaidia na wengine.” Mali zinazodaiwa kuachwa na marehemu ni pamoja na mashamba makubwa, nyumba karibu kumi, matrekta na biashara nyingine mbalimbali.
na libeneke blog

0 comments:

Post a Comment