.

.
Friday, May 2, 2014

3:15 AM

Mwenge wa uhuru. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Gharib Bilal, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2014, katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, mkoani Kagera Mei tarehe 2 mwaka huu.


Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella Mukangara wakati akiongea na Waandishi wa Habari Mjini Bukoba kuhusu Mbio hizo.

Mwenge huo utakaobeba ujumbe usemao “Katiba ni Sheria Kuu ya Nchi” wenye kauli mbiu “Jitokeze kupiga kura ya maoni tupate Katiba Mpya”utakimbizwa katika Halmashauri/Manispaa 165 za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kilele chake kitakuwa Mkoani Tabora tarehe14/10/2014.


Ujumbe kuhusu mabadiliko ya Katiba kwa mwaka huu, umeandaliwa mahususi kwa lengo la kuwahimiza wananchi kuendelea kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa ambao mwisho wake ni wananchi kupiga kura ya maoni ili tupate Katiba Mpya iliyoboreshwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Amesema Dkt. Mukangara.


Amesema kuwa ujumbe huu utaambatana na kauli za uhamasishaji kuhusu mapambano dhidi ya UKIMWI, Malaria, Rushwa na Matumizi ya Dawa za Kulevya.

Dkt. Mukangara ameeleza kuwa nchi yetu bado inakabiliwa na changamoto ya ugonjwa hatari wa UKIMWI, Malaria, matumizi ya dawa za kulevya na rushwa, hivyo mwaka huu kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru Serikali itaendelea kuwahimiza wananchi kupambana kwa dhati ili kumaliza changamoto hii inayoathiri maisha ya Watanzania.

“Hata hivyo, Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na kuendelea kuhimiza umuhimu wa amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa; Serikali kupitia Mbio hizi imekuwa ikiwahamasisha Wananchi, Mashirika, Taasisi na Wadau mbalimbali kuchangia kwa hali na mali kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo”. Amesema Dkt. Mukangara.

Amekumbusha kuwa falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni kumulika maovu ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu, kuleta matumaini ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki,heshima palipojaa dharau.

0 comments:

Post a Comment