.

.
Thursday, May 8, 2014

12:10 PM

TIMU ya JKT Oljoro imepania kukabili ushindani wa ligi Daraja la Kwanza kwa kuanza maandalizi mapema ikiwemo kuingia kambini na kujifua kwa mazoezi magumu ili waweze kurejea Ligi Kuu ya Vodacom.
JKT Oljoro imeshuka daraja msimu huu baada ya kudumu Ligi Kuu kwa takribani miaka minne.
Akizungumza, Mwenyekiti wa timu hiyo, Meja Sijaona Myala, alisema kuwa timu itaingia kambini Mei 25 na watajifua kisawasawa mfululizo, sambamba na mechi mbalimbali za kirafiki.
“Suala la kushuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi Daraja la Kwanza halitukatishi tamaa, bali ni kuangalia tu yapi yalisababisha ili turekebishe na changamoto ni zipi tuzitatue ili kuhakikisha tunapanda na kubaki juu, kwa sababu hata sisi tuko fiti kisoka na wapinzani wetu wanatukubali,” alisema.
Alisema kwa sasa wanachokifanya ni kuboresha timu, benchi la ufundi na kutafuta makocha wa makipa, sambamba na kuziba mapengo ya wachezaji waliomaliza mikataba, yote ikiwa ni mikakati ya kutimiza malengo waliyojiwekea ya kupanda na kubaki kung’ara kwenye soka.
Katika hatua nyingine, uongozi huo pia umejipanga kuboresha michezo mingine kama netiboli, ngumi, riadha, wavu n.k.

0 comments:

Post a Comment