.

.
Sunday, May 11, 2014

10:00 PM

Lanjui aliyelazwa katika Wodi Namba Nne katika hospitali hiyo tangu Januari Mosi, 1971, awali alilazwa katika Hospitali ya Sekou Toure, Mwanza kuanzia mwaka 1969 mara baada ya kupata ajali.
Siku mbili zilizopita tulichapisha picha na habari katika ukurasa wa mbele wa gazeti hili kuhusu mgonjwa anayejulikana kwa jina la Abdi Lanjui ambaye amelazwa wodini katika Hospitali ya Singida kwa miaka 45 sasa, kutokana na ajali mbaya aliyopata mwaka 1971. Mgonjwa huyo mwenye miaka 75 alikuwa dereva wa Mamlaka ya Pamba na kupata ajali hiyo mkoani Mwanza baada ya lori alilokuwa akiendesha kuchomoka gurudumu la mbele na kupinduka.
Kusikiliza maelezo yake kuhusu mkasa huo uliompata kunatia uchungu mkubwa. Maelezo yake yanaleta hisia kwamba dunia siyo tu haina huruma, bali pia ni katili na ndiyo maana imemsahau na kumtosa kwa muda mrefu hivyo. Jambo la ajabu ni kuwa, ni mtulivu na mvumilivu kwa kiwango cha juu na bado anaishi kwa matumaini. Hana hasira wala kinyongo na dunia au jamii iliyomwacha katika upweke na maumivu makubwa kwa miaka yote hiyo 45.
Akizungumza huku akionekana kuwa katika mateso makubwa, anasema sababu ya kugeuza wodi kuwa makazi yake ya kudumu ni ajali iliyomsababishia kupooza kuanzia kiunoni hadi kwenye nyayo. Anasema kwa kuwa hanyanyuki kitandani, amepata vidonda kuanzia makalioni hadi miguuni na kuongeza kwamba anaishi maisha magumu mno.
Kutokana na hali hiyo, anaiomba Serikali na jamii kwa jumla imwonee huruma kwa kumsaidia chakula kwa kuwa hana ndugu wa kumpatia msaada wowote. Anasema, kwa miaka mingi uongozi wa hospitali ya Mkoa ulikuwa ukimhudumia kwa kumpa chakula, lakini baadaye huduma hiyo ilisitishwa, hivyo kumfanya awe ombaomba na maisha yake kuwa ya mlo mmoja kwa siku.
Kwa kuwa hawezi kunyanyuka kitandani na hana ndugu yeyote, amekuwa akiwaomba msaada manesi na watumishi wengine wa hapo hospitalini. Anawashukuru kwa kufanya hivyo bila kuchoka na kumwezesha angalao kupata mlo mmoja kwa siku, lakini pia anaomba msaada wa fedha ili aweze kwenda Hospitali ya KCMC au hospitali nyingine yoyote inayofaa ili apate huduma zaidi ya matibabu.
Mgonjwa huyo aliyelazwa katika Wodi Namba Nne katika hospitali hiyo tangu Januari Mosi, 1971, awali alilazwa katika Hospitali ya Sekou Toure, jijini Mwanza kuanzia mwaka 1969 mara baada ya kupata ajali. Akiwa katika hospitali hiyo mwishoni mwa mwaka 1970, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya na ndipo alipomwomba mwajiri wake amrudishe nyumbani katika Kijiji cha Mhintiri katika Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida mwaka 1971. Bahati mbaya ni kuwa, wakati anapata ajali na kulazwa hospitalini, wazazi wake na ndugu yake pekee walikuwa tayari wamefariki dunia.
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Mussa Kamala anasema hivi sasa mgonjwa huyo anahudumiwa na hospitali kama watu wengine wenye ulemavu. Anasema uongozi wa hospitali hiyo uliwahi kumkabidhi kwa Idara ya Ustawi wa Jamii ili ifanye mpango wa kumrudisha nyumbani, lakini haikuwezekana.
Wakati huohuo, Ofisa Ustawi wa Jamii mkoani Singida, Zuhura Kalya anasema walishindwa kumrejesha nyumbani kwao, kwani walipofuatilia ilibainika kwamba hana ndugu na hakukuwa na mtu anayemfahamu kwa kuwa aliondoka kijijini hapo mwaka mmoja baada ya Uhuru.
Sisi hatuna la zaidi, isipokuwa kuwaomba wananchi kumsaidia mgonjwa huyo ambaye ameteseka vya kutosha kwa takribani nusu karne sasa. Ni matumaini yetu kwamba Serikali pia itachukua hatua stahiki haraka iwezekanavyo.

0 comments:

Post a Comment