.

.
Thursday, May 8, 2014

12:07 PM
KOCHA maarufu wa riadha, Samwel TupaKOCHA maarufu wa riadha, Samwel Tupa, ameulalamikia uongozi wa Riadha Tanzania (RT), kwa kutumia jina lake kama kocha aliyeondoka na wanariadha waliokwenda nchini New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya Jumuiya ya Madola yanayotarajia kufanyika Glasgow, Scotland, Julai mwaka huu.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa jijini Arusha, Tupa alisema hajui sababu iliyofanya uongozi huo kufanya hivyo, na kwamba mara ya mwisho aliwasiliana na Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui, ambaye alimtaka wabaki ili waandae mashindano ya taifa yanayotarajiwa kufanyika Juni.
“Nyambui aliponiambia hivyo, nilimwambia mimi kama kocha siwezi nikabaki wakati wanariadha wangu wanakwenda, huko watafundishwa na nani, akadai watakuwa na kocha wa China, lakini mimi sikuafiki hilo na nikajua watakuwa wamebadilisha jina la kocha anayeenda, ila cha kushangaza naona kwenye vyombo vya habari kwamba nimeenda huko,” alisema.
Alisema mbali na yeye kuachwa, pia wamemuacha mwanariadha mwingine, Michael Damson, ambaye naye alikuwepo katika orodha ya kwenda na aliambiwa apeleke pasipoti, ila kaachwa bila taarifa yoyote.
“Baniani mbaya kiatu chake dawa na kidole kidogo kinashika mpini wa jembe, lakini hakiingii kwenye bakuli ya mboga, mimi siwezi kulalamika sana, lakini ninachohoji kwanini watangaze jina langu kwamba nimekwenda wakati nimeachwa bila kupewa taarifa yoyote?” alihoji kocha huyo wa kimataifa ambaye ni mkufunzi pekee Tanzania wa mchezo huo aliyethibitishwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).
Alisema kwa kuonyesha kwamba uongozi huo unakubali kazi zake, waliamua kuondoka na mwanariadha wake, Michael Gwandu bila kumpa taarifa na kuamua kuwasiliana na kocha msaidizi.
Alipotafutwa Rais wa RT, Anthony Mtaka, alitaka atafutwe makamu wake,  William Kallaghe, ambaye alidai ahusiki na benchi la ufundi, hivyo atafutwe Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Ombeni Zavalla, ambaye pia alisema anayejua utaratibu wa safari hiyo ni Nyambui, yeye hajui lolote

0 comments:

Post a Comment