.

.
Friday, May 2, 2014

3:36 AM
Mbowe, Profesa Lipumba, Mchungaji Mtikila wahutubia.

ZANZIBAR. 
Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameapa kuendelea kudai mfumo wa Muungano wa serikali tatu nje ya Bunge la Katiba kwa nguvu zote, ikiwamo kufanya maandamano ya amani nchi nzima.
Msimamo huo ulielezwa na viongozi hao kwa nyakati tofauti katika mkutano wa hadhara uliofurika mashabiki kwenye Viwanja vya Kibandamaiti, Unguja jana.


Mwenyekiti Ukawa, Freeman Mbowe alisema wameamua kuliacha Bunge la Katiba kutokana na harufu za rushwa, vitisho na matusi huku baadhi ya wabunge wakiahidiwa vyeo. Mbowe ambaye hata hivyo hakufafanua zaidi, alisema Ukawa wameamua kwenda kwa wananchi kuwaeleza dhamira chafu walionayo wabunge wa CCM katika mpango wao wa kukataa Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba.


“Ni jambo la hatari katika mchakato wa Katiba wananchi kuwa waoga au hofu... Lazima tuwe tayari kuwaonyesha watawala kuwa tuna umoja imara, tunayapigania mataifa huru ya Tanganyika na Zanzibar, Rais Kikwete (Jakaya) asiwatishe wananchi kwa kivuli cha jeshi kuchukua madaraka,” alisema Mbowe.


Lipumba anena
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba alisema wajumbe wa Ukawa wameamua kujitoa bungeni kutokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete ambayo alidai kuwa iliibeza na kuidhalilisha Tume ya Warioba.


Alisema hawatarudi bungeni na kwamba hawawezi kujadili Katiba ambayo siyo maoni ya wananchi.


Alidai kwamba kwa makusudi Rais Kikwete aliamua kutetea sera za chama chake na kupingana na maoni yaliyotolewa na wananchi kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba.


“Rais Kikwete ameharibu nia ya kupatikana Katiba Mpya, amekuwa akijulishwa kila hatua na jinsi maoni ya wananchi walivyokuwa wakipendekeza serikali tatu katika Rasimu ya Kwanza na ya Pili naye akawa anaafiki, inashangaza amegeuka na kukataa maoni ya wengi,” alisema Profesa Lipumba.


Mtikila akumbushia jela
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alisema aliwahi kufungwa jela mara tatu, kuwekwa mahabusu mara 43 kwa kudai lipatikane Taifa la Tanganyika huku watawala wakikataa matakwa ya wengi kwa sababu na hoja dhaifu.


Mchungaji Mtikila aliongeza kusema kwamba wanachokitaka CCM na Serikali zake ni kuendelea kuwabana wananchi wa Tanganyika na Zanzibar wasiweze kuwa huru na kujivunia mataifa yao.


MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment