.

.
Thursday, May 29, 2014

Hanang. 
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana amesema wawekezaji kutoka nje walioshindwa kuyaendeleza mashamba ya ngano ya Bassotu na Wareti, wilayani Hanang mkoani Manyara, watanyanganywa mashamba hayo.
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo juzi kwenye mji mdogo wa Katesh baada ya kupokewa kutoka mkoani Singida, Kinana alisema atalifikisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete ili mashamba hayo yarudishwe kwa wazawa.
Inadaiwa kuwa wawekezaji kutoka nje, ikiwamo kampuni moja ya Kenya, imekuwa ikiwakodisha wananchi mashamba hayo kulima mahindi badala ya wao kulima ngano kama mkataba ulivyosainiwa.
“Hatuwezi kukubali kuwavumilia wawekezaji walioshindwa kuendeleza mashamba waliyopewa na badala yake wanawakodisha wananchi wetu...sasa nini maana ya uwekezaji wenye tija?,” alihoji Kinana.
Alisema kuwa atalifikisha suala hilo kwa Rais Kikwete ili wawekezaji hao wanyang’anywe na kupewa wakulima wa maeneo ya Hanang’.
Aliongeza: “Mashamba haya lazima yarudishwe kwa wananchi kama wawekezaji wameshindwa kutimiza masharti ya mkataba kulima ngano.”
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rose Kamili aliwahi kumwomba Rais Jakaya Kikwete kuwanyang’anya wawekezaji hao mashamba kwa vile wamekiuka taratibu na kuwakodisha wananchi.
Kamili alitoa ombi hilo wakati Rais Kikwete alipofanya ziara mkoani Manyara, Desemba mwaka 2012.
“Tunataka mashamba ya ngano yaendelee kulimwa ngano na siyo wawekezaji kuyakodisha kwa wananchi ambao wanalima mahindi,” alisema Rais Kikwete katika ziara hiyo.

0 comments:

Post a Comment