.

.
Friday, May 2, 2014

3:51 AM


Rais Jakaya Kikwete akiangua kicheko wakati walimu (juu), walipokuwa wakipita kwa maandamano, huku wakiimba ‘Shemeji mshahara bado’ wakati wa sherehe za Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) zilizofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam jana. Walimu walimwita shemeji kwa kuwa mkewe, Salma ni mwalimu kitaaluma. Picha na Silvan Kiwale.

Dar/mikoani.
Rais Jakaya Kikwete ametoa ahadi mbili za kuwafurahisha wafanyakazi. Kwanza ametangaza nia ya kuongeza mishahara yao na pili, kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara hiyo mambo ambayo ameahidi kutekelezwa katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni hivi karibuni.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema anatambua kuwa wafanyakazi wana hamu ya kujua Serikali itasema nini kuhusu masilahi yao.
Alisema malalamiko ya wafanyakazi wengi ni kutaka kuona kima cha chini cha mshahara kinaongezwa huku kodi kwenye mishahara (Paye), ikipungua.
“Mimi na wenzangu serikalini hatuna upungufu wa dhamira ya kufanya hivyo, tumethibitisha miaka iliyopita na tutaendelea kuwa hivyo,” alisema.
Huku akishangiliwa na wafanyakazi waliofurika katika Uwanja wa Uhuru, Rais Kikwete alisema: “Najua kuwa nyongeza tuliyotoa mwaka jana si kubwa kama wafanyakazi walivyotaka iwe... hata mimi nisingependa iwe hivyo.”
“Kwa nyongeza iliyofanywa mwaka jana, hivi sasa Serikali inatumia asilimia 44.9 ya Bajeti kulipa mishahara ambayo ni asilimia 10 ya Pato la Taifa.”
Akifafanua namna Serikali ilivyofikia uamuzi wa kuongeza mishahara kwa mwaka huu, Rais Kikwete alisema kulikuwa na mjadala mkali baina ya wafadhili waliodai nyongeza ni kubwa mno.
“Ni kweli mapato yetu ni madogo lakini kwa kuwa mishahara ni midogo, lazima tuendelee kuongeza, hata hicho kidogo lazima ukitoe ili uijenge ile nafuu, alisema bila kutaja kiwango kitakachoongozwa.
“Hata sasa kumekuwa na ubishi mkali kati ya Wizara ya Utumishi na Hazina kuhusu nyongeza ya mwaka huu iwe mpaka kiasi gani, nikaingilia kati nikakubaliana na utumishi, Hazina walikuwa wanataka ipingue kidogo,” alisema.
Walimu na shemeji yao.
Suala la mshahara lilijitokeza kwa namna nyingine kwenye maandamano ya wafanyakazi pale walimu walipoamua kusimama mbele ya jukwaa kuu na kumweleza Rais Kikwete ambaye walimtaja kama shemeji yao, kwamba hawajapata mshahara wa Aprili wakimtaka aingilie kati.
“Shemeji, shemeji, shemeji, hatujapata mishahara yetu ya Aprili, tunaomba utusaidie,” walitoa ujumbe huo kwa njia ya wimbo
 
.MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment