.

.
Friday, May 2, 2014

Na Bertha Mollel --Arusha
TIMU ya AFC ya Arusha imepokea msaada wa vifaa vya michezo zikiwemo jezi, mipira na viatu vyote vikiwa na thamani ya sh milioni 2.5 kutoka Kampuni ya Tanzanite Forever ikiwa ni sehemu ya kuiwezesha kushiriki ligi ya mabingwa wa mikoa itakayoanza Mei 10, mwaka huu jijini Mbeya.
Pamoja na vifaa hivyo, kampuni hiyo imebeba jukumu la kugharamia nauli na mahitaji yote ya timu hiyo kwa muda wote itakayokuwa ikishiriki ligi hiyo, ukiwa ni mkakati wa kuirejesha Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushuka daraja miaka minne iliyopita.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzanite Forever, Faisal Shahbhai, alisema umefika wakati sasa kwa wapenzi na wadau wa soka kujiunga pamoja kusapoti mpira wa Mkoa wa Arusha na kuelekeza nguvu kubwa katika kuichangia kwa hali na mali AFC ambayo ndiyo yenye wapenzi wengi mkoani hapa.
Shahbhai alisema kuwa, AFC inahitaji sapoti kubwa ili iweze kushiriki ligi ya mabingwa wa mikoa na kushika nafasi ya kwanza na kupanda Daraja la Kwanza, hatua moja kabla ya kurejea Ligi Kuu na kwa sasa inahitaji fedha kwa ajili ya kulipa hoteli, posho za wachezaji na chakula kipindi chote watakachokuwa Mbeya.
Aliongeza kuwa, wachezaji wa AFC wameonesha moyo wa kujituma na kujitolea kuanzia Ligi ya Wilaya hadi Mkoa na sasa ni wakati wa wadau na wahisani mbalimbali, kuisaidia ili iweze kuukomboa Mkoa wa Arusha ambao hauna timu ya Ligi Kuu kwa sasa, baada ya Oljoro JKT iliyokuwa ikishiriki ligi hiyo kwa miaka mitatu, kushuka daraja mwaka huu.
Akipokea vifaa hivyo, Katibu Mkuu wa AFC, Mike Warioba, alitoa rai kwa wachezaji kuonyesha shukrani kwa kufanya vizuri katika ligi hiyo na kusahau hali ngumu iliyokuwa ikiikabili na kubeba jina la timu hiyo inayosifika na kuogopwa na timu nyingi kongwe hapa nchini.

0 comments:

Post a Comment