.

.
Tuesday, February 3, 2015


http://jumamtanda.blogspot.com

Bondia Francis Cheka akiwa chini ya ulinzi huku akisindikizwa kuingia katika mahabusu baada ya kuhukumiwa jela miaka mitatu na kulipa fidia kiasu cha sh1,000,000/= kufuatia mahakama ya hakimu mkazi Morogoro kumtia hatia kwa kosa la kumshambulia meneja wake mkoani Morogoro. Picha Juma Mtanda.

Bondia wa ngumi za kulipwa duniani Frances Cheka (32) amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa fidia ya Sh. 1 milioni baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumpiga meneja wake wa baa na kwamba hukumu hiyo imemfanya mke wake aangue kilio kizito mahakamani baadhi ya watu wakidai adhabu hiyo ni kubwa kulingana na kosa na imetokana na bondia huyo kushindwa kujitetea baada ya kupatiwa fursa hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya mkoa wa Morogoro, Said Msuya baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ambao haukuacha shaka yoyote katika kuthibitisha shtaka hilo.


Akisoma hukumu hiyo hakimu huyo alisema kuwa adhabu hiyo itakuwa fundisho kwa mshtakiwa na watu wengine wanaotumia vibaya nguvu zao na kwamba mshtakiwa anatakiwa kumlipa fidia ya Sh. 1 milioni kwa mlalamikaji.


Hata hivyo Cheka alipewa nafasi ya kujitetea ili mahakama impe adhabu ya huruma hata hivyo aliieleza mahakama kuwa hana maelezo yoyote ya kujitetea zaidi ya kuiachia mahakama kuamua adhabu itakayompa.


Mara baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo mke wa Cheka ambaye alishindwa kutaja jina lake kutokana na kilio alidai kuwa mumewe ameonewa na kwamba hakustahili kupewa adhabu hiyo.


Katika hali ya kushangaza kabla na baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo Cheka ambaye ni bondia wa dunia ambaye pia ni maarufu hapa nchini alionekana akiwa na mke wake huku wapenzi wengi wa ngumi mkoani hapa wakiwa hawana taarifa za hukumu hiyo.Awali ilidaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashtaka wa Polisi Anganile Nsiyani kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 2 mwaka 2014 katika baa ya Vijana Social Hall iliyopo Manispaa ya Morogoro.


Mwendesha mashtaka huyo alidai kuwa bila halali na akijua kufanya hivyo ni kosa Cheka alimshambulia meneja wake wa baa aliyefahamika kwa jina la Bahati Kibanda kwa kumpiga ngumi usoni na tumboni na hivyo kumsababishia maumivu makali.


Alipofikishwa mahamani hapo kwa mara ya kwanza Cheka alikana shtaka hilo na hivyo upande wa mashtaka uliamua kupeleka mashahidi wanne kati ya saba ambao waliithibitisha mahakamani hapo bila ya shaka kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo na hivyo mahakama kumtia hatiani.

0 comments:

Post a Comment