.

.
Wednesday, February 25, 2015

2:43 AM
Halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro imetupia lawama Chama cha soka mkoa wa Arusha (ARFA) kukataa kuruhusu wilaya hiyo kushiriki kwenye mashindano ya ligi kwa madai ya kutokutambua uongozi wa soka.

Akizungumza na gazeti hili Afisa utamaduni na michezo wa wilaya hiyo Bakari Gaima alisema kuwa wamekuwa na kiu kubwa ya kushiriki ligi za taifa ili kuonyesha uwezo wao katika kusakata soka lakini wamekuwa wakinyimwa haki hiyo na uongozi wa chama cha soka mkoa.

“Jamani ninyi mlioko karibu na mjini tusaidieni huku sisi tunanyimwa haki zetu za kucheza mpira na kila tukitaka tushiriki ligi kwa kuandaa timu bingwa wa wilaya yetu anakataliwa kwa madai kuwa sisi hatuna hatuna chama sasa tunachoshindwa kuelewa ni chama kipi hicho wakati tuna uongozi??”

“Mwanzo Katibu wa soka mkoa alisema kuwa wilaya yetu hatuwezi kushiriki ligi kwa sababu hatuna uongozi hivyo tukaamua kufanya uchaguzi wa kuwachagua viongozi wetu wa soka na tukafanya ligi ya wilaya lakini tulipopeleka jina mwaka jana tukaambiwa uongozi wetu ni batili kwa kuwa hatujazingatia kanuni za katiba mpya zilizotolewa na TFF”

“Hata hivyo tukaamua kutaka ujua kanuni mpya za TFF tukaambiwa kuwa katibu huyo atakuja kutuletea katiba hiyo na kuisoma tuielewe na kuzindua chama cha soka ambayo hiyo itakuwa tiketi ya sisi Ngorongoro kushiriki ligi lakini unaambiwa hadi leo hakuna kilichofanyika hadi leo na bado tunaambiwa hatuna sifa”

“Mwaka jana kabla ya ligi ya mkoa kuanza tulikwenda hadi mjini ambayo ni zaidi ya kilimeta 430 kufuata hiyo katiba mpya maana tunaona tunacheleweshwa kushiriki ligi lengo ni tufuate taratibu hizo tufanye uchaguzi na bingwa wetu wa wilaya akachuane mkoani lakini cha kushangaza chama cha soka mkoa ulitunyima katiba hiyo kwa madai watakuja wenyewe hadi leo hatujawaona, jamani mbona mnatutenga?? Alilalama Afisa michezo Gaima.

Alisema kuwa mabingwa hao wa wilaya ilishindikana kushiriki ligi hiyo hadi leo wanasubiri huku ligi ya mkoa imefikia hatua ya sita bora huku wakilalama kuwa wamekuwa wakitengwa tangu kuanzishwa kwa wilaya hiyo kwani hata mashindano ya copacocacola walitakiwa kuandaa timu lakini wakashindwa kupewa taarifa ni lini kuleta timu hiyo kucheza hadi mda ukapita.

Kwa upande wake katibu wa soka mkoa wa Arusha Adam Brown alikanusha kuwatenga kisoka wilaya hiyo huku akisema kuwa mfuko wa mkoa kwa sasa hauna fedha hivyo wanasubiri hadi ipatikane wapate kwenda kuzindua chama hicho na kuwasomea katiba mpya ya Shirikisho la soka.

“Unajua wilaya ile iko mbali ndio maana unashindwa kwenda bila kuwa na pesa hivyo tunajipanga kama hela ikipatikana tutakwenda na sio kweli kwamba tunawatenga ila tumewaambia hawawezi kushiriki ligi bila kuwa na chama kinachotambulika na TFF na kama wakikamilisha hilo Afisa michezo ataitisha kamati na kufanya uchaguzi” alisema Brown.

0 comments:

Post a Comment