.

.
Wednesday, February 25, 2015

3:17 AM
 

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM (CC) inakutana Jumamosi wiki hii huku mambo muhimu sita yakitarajiwa kujadiliwa, likiwamo suala la makada wa chama hicho waliopewa adhabu ya onyo kali kwa kuanza kampeni za urais mapema na ukiukaji wa maadili.


Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, licha ya kutoeleza ajenda za kikao hicho, ilisema kitafanyika jijini Dar es Salaam na kuongozwa na mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kuanzia saa 4 asubuhi.


Kikao hicho kinafanyika wakati upepo wa kisiasa ndani ya chama hicho ukiwa haujatulia huku kukiwapo masuala mazito ya kitaifa yanayotikisa medani za kisiasa, likiwamo suala la uandikishaji wapiga kura, maandalizi ya kura ya maoni za kupitisha Katiba Inayopendekezwa na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, ambayo yameelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa hayawezi kukwepeka katika kikao hicho.


Adhabu kwa wagombea
Itakumbukwa kuwa kikao hicho kitafanyika ikiwa ni siku 10 baada ya kukamilika tarehe ya mwisho ya adhabu kwa makada sita wa CCM, waliokuwa wakitumikia adhabu ya miezi 12 kwa ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa na CCM kugombea urais.


Kikao kilichopita cha CC kilichoketi Januari 13, mwaka huu kilibainisha kuwa baada ya muda wa adhabu zao kuisha, Kamati Kuu ingefanya tathimini kuona iwapo wagombea hao walizingatia masharti ya adhabu zao na endapo kungekuwa na ambao hawakuzingatia masharti adhabu zao zingeongezwa.


Wiki iliyopita, Nnauye alithibitisha kuwa muda wa adhabu hiyo ulikuwa ukingoni na kuwa viongozi hao wangefanyiwa tathmini na kamati ndogo ya maadili ili kubaini iwapo adhabu hiyo ilitekelezwa ipasavyo.


Makada waliokuwa wakitumikia adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.


Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.


Kikao hicho huenda pia kikazungumzia mwenendo wa uandikishaji wa wapiga kura katika Daftari la Kudumu kwa kutumia teknolojia ya alama za vidole (BVR), iliyozinduliwa jana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.


CCM, ni miongoni mwa vyama vya siasa nchini vinavyoungana na vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuhoji mara kwa mara ufanisi wa mfumo wa BVR katika kuandikisha wapigakura kutokana na historia yake isiyoridhisha.


Wachambuzi
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema anaamini CC itajadili pamoja na mambo mengine, matokeo ya Kamati ya ndogo ya maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Philip Mangula, iliyojadili suala la wagombea na kashfa ya Tegeta Escrow.


Dk Bana alitolea mfano suala la kashfa ya ufisadi katika Akaunti ya Escrow kuwa ni suala mbalo CCM wanaweza wakaamua kulibeba kama hoja na kuyapeleka kwa ajili ya kujadiliwa na kikao hicho kikubwa cha chama.


“Hili suala la ufisadi wa Tegeta Escrow ni ‘critical issue’, ni muhimu kwa chama chao kulijadili na kuja na majibu ya maswali yanayowasumbua wananchi wengi, hasa ukizingatia kuwa suala hilo lilikitikisa sana chama hicho,” alisema Dk Bana.


Alisema jambo lingine linaloweza kuchukuliwa kama ajenda katika kikao hicho na kuamua kulijadili ni wale wanachama wake waliojitangaza kugombea urais na ambao waliopewa adhabu ya mwaka mmoja ambapo anasema wanaweza kutaka kufanya mapitio, kama walitekeleza maagizo


“Vile vile wanaweza kuangalia kalenda ya uchaguzi ya chama chao na wajadili na kupendekeza utaratibu wa jinsi ya kuwapata wagombea wao…vile vile lipo suala la hali ya siasa nchini, hali imebadilika, upepo hauvumi kuelekea CCM,” alisema.


Aliongeza kuwa masuala mengine wanayoweza kujadili ni matukio ya kutisha na yasiyo ya kawaida yanayojitokeza nchini kama vile matukio ya kutekwa kwa watu na kuteswa, kuibuka kwa panya road na mengine yanayofanana na hayo ambayo anasema ni ukweli ulio wazi kuwa matukio hayo yanaashiria kuvurugika kwa amani na utulivu wa nchi.


“Matukio mengi yasiyo ya kawaida yameibuka hivi karibuni, mfano suala la vijana wa JKT nao wanaandamana wanataka ajira, lakini kila mtu anajua kuwa wale vijana wanajulikana wanafundishwa kujenga nidhamu, sasa wanaandamana, kunaonekana lipo tatizo nchini. Yote haya hayaleti mwelekeo mwema kwa jamii,” alisema.


Aliongeza kuwa, “tuhuma nzito zinazowakabili wanachama wake wanajua madhara yake na wanajaribu kutaka kuyarekebisha ili kurejesha ushindi ambao kwa kweli unaonekana kuwaendea vibaya. Haya yote yanaweza kuwasukuma kuitisha vikao nyeti kama hivi na kujadili mustakabali wa chama chao ili waendelee kupata ushindi wa kishindo.


Alisema kitu kingine muhimu ambacho hawawezi kukikwepa kukijadili ni pigo walilolipata katika chaguzi za serikali za mitaa, ambapo chama hicho kilionekana kupata anguko kubwa kuliko matarajio.


Mengine aliyosema yanawezwa yakawa ajenda katika kikao hicho ni pamoja na kura ya maoni ya Katiba iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu, muda anaosema hata wana CCM wenyewe wanajua kuwa hautoshi.


Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alisema kubwa ambalo CCM linalowahangaisha na ambalo kwa namna yoyote huenda likawa miongoni mwa ajenda katika kikao chao ni kuleta utulivu wa ndani ya chama na kumjua mwanaCCM atakayepeperusha bendera yao.


“Nadhani hata wale wanachama wake sita waliopewa adhabu bado hawajaelezewa kama adhabu zao zimekwisha. Ingawa muda wa adhabu umekwisha, lakini hawajaelezwa hatma yao, kwa hiyo hili ni jambo muhimu ambalo hawawezi kuliacha.


Mbunda alisema jambo lingine muhimu kabisa ambalo huenda itapewa uzito ni hili la kumpata mgombea anayekubalika katika jamii na ambaye ataweza kupeperusha vyema bendera ya chama na kukubalika na makundi yote.


“CCM waliozoea kuwa hakuna sababu ya kuangalia ni mgombea gani anayekubalika na jamii kwa imani kuwa wakisimamisha yeyote atapita, hali ya sasa kwa namna yoyote lazima waweke mtu anayekubalika katika jamii na hii ni ajenda kubwa inayohitaji mjadala mpana.


“Na ile tabia ya kutengeneza mazingira fulani awepo na huyu asiyepo, lazima waichukulie kwa uangalifu,” alisema Mbunda.


Mbunda alisema jambo lingine ni suala la kura ya maoni ya Katiba, ambalo pia ni suala nyeti na muhimu kwa CCM na kuwa wanapaswa wajipange vyema endapo wanataka Katiba waliyoipendekeza ipite


.MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment