.

.
Wednesday, April 10, 2013

4:48 AM
 
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MOROGORO FAUSTINE SHILOGILE.
 
ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kikosi cha Kizuka Wilaya ya Morogoro Vijijini mwenye cheo cha Koplo, Kurwa Juma (41) amekutwa amekufa chumbani kwake baada ya kujinyonga na mkanda wa begi la nguo.
Kwa Mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Faustine Shilogile, tukio hilo lilitokea Aprili 8 mwaka huu, saa 6 mchana maeneo ya Kingolwira, katika Manispaa ya Morogoro.

Alisema mtoto wa marehemu aliyemtaja kwa jina la Rajabu Kurwa (13), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kingolwira ndiye aliyegundua kuwa baba yake amejinyonga kwa kutumia mkanda wa begi la nguo chumbani kwake, huku chanzo cha kujinyonga kikiwa bado hakijafahamika.

Wakati huo huo, wanafunzi wa Shule ya Mtakatifu Martin iliyopo katika kijiji cha Mbingu, Tarafa ya Mngeta wilayani Kilombero, wamenusurika kufa baada ya bweni lao kuteketea kwa moto.

Kamanda huyo alisema tukio hilo lilitokea Aprili 8, mwaka huu, saa 12:30 asubuhi, katika shule hiyo iliyopo kijiji cha Mbingu, ambapo paa la bweni hilo na vifaa vya wanafunzi viliteketea vyote kwa moto.

Alisema watu wasiofahamika walilichoma moto bweni hilo, lakini hakuna mtu aliyejeruhiwa kwenye ajali hiyo ambapo thamani ya vifaa vilivyoteketea bado haijafahamika.

Hata hivyo alisema chanzo cha kuchoma bweni hilo bado hakijajulikana na polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini wahusika.

0 comments:

Post a Comment