Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani hapa limesema litaendelea kushirikiana
na mashirika mbalimbali katika kulinda na kutetea haki za watoto. Hayo
yalisemwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Mary Lugola ambaye pia ni Mkuu wa
Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa
maadhimisho ya siku ya mtoto wa mtaani duniani.
Katika maadhimisho hayo ambayo yalifanyika tarehe 12 mwezi
huu katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini hapa, Mrakibu huyo Mwandamizi wa
Polisi alisema kwamba jeshi la polisi kupitia dawati la jinsia na watoto mkoani
hapa limekuwa karibu sana kiutendaji na mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya
serikali kama vile Mkombozi, CCR, Action For Children n.k katika kutetea na
kulinda haki za watoto wa mitaani.
Mrakibu huyo Mwandamizi wa Polisi ambaye pia ni Mkuu wa
Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha alisema mbali na jeshi hilo kujihusisha
katika kutetea na kulinda haki za watoto wa jamii hiyo, pia linasaidia kuinua
na kuibua vipaji vya watoto hao kupitia programu ya MWONGORIKA ya Polisi jamii
ambayo inajihusisha na michezo kwa vijana.
Alisema kupitia Dawati hilo, jeshi la polisi limeweza
kuwahudumia watoto wa mitaani kwa kushirikiana na mashirika hayo ili
kuwawezesha waishi katika mazingira salama na kupata mahitaji muhimu.
“Kwa mfano tumeshawahi
kuwaunganisha na wazazi wao pamoja na kuwasafirisha kwenda makwao watoto
waliokuwa tayari kurudi ”. Alisema Bi. Lugola.
Alimalizia kwa kusema kwamba Dawati la Jinsia na watoto huwa
linahakikisha linapata taarifa za watoto walioathirika na pia wale wote
wanaowanyanyasa watoto hao wanachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa
mahakamani.
Nalo shirika la Mkombozi kupitia risala yao iliyosomwa na
Afisa Ustawi wa Jamii wa Shirika hilo Bi. Doris Cornell alisema kwamba ujumbe
wa mwaka huu katika kuadhimisha siku hiyo ni “Nyumbani Mtaani Nyumbani” ikiwa
na maana ya kwamba, mtoto atatoka nyumbani kwenda mtaani na kisha atarudi
nyumbani.
Alisema lengo la siku hiyo ni kuwapa jukwaa watoto waishio na
kufanya kazi mtaani wakiungana na wengine duniani kote kupaza sauti ili haki
zao zisiipuzwe.
Bi. Doris alisema watoto waishio mitaani na kulala mitaani
wanazofursa na haki sawa na watoto wengine duniani na kwamba wana haki ya
kuishi, kulindwa, kuendelea na kushiriki katika mambo yanayogusa maisha yao
kama ilivyoainishwa katika mkataba wa Kimataifa wa haki za watoto kifungu cha
4.
Risala hiyo ilieleza sababu za kuwepo kwa watoto hao mitaani
ni pamoja na kukosa haki za msingi (chakula, malazi, mavazi, ulinzi, elimu,
upendo, matibabu n.k) kutoka katika familia zao, kufiwa na mzazi mmoja au wote
wawili,
Sababu nyingine ni vitendo vya unyanyasaji na ukatili
waliofanyiwa katika jamii au familia, kipato duni katika familia/wazazi/walezi,
utumikishwaji wa watoto (ajira za watoto), kubaguliwa na kunyang’anywa mali za
wazazi wao.
Siku hiyo ambayo huwa inaadhimishwa katika nchi 130 duniani,
Tanzania na Uingereza ikiwa ni miongoni mwa nchi hizo, ilihudhuriwa pia na
viongozi mbalimbali wa ngazi ya wilaya pamoja na Mkuu wa Dawati la Jinsia na
Watoto Mkoa wa Arusha Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Maria Maswa.
0 comments:
Post a Comment