WANASIASA wawili vijana
ambao wamekuwa katika vita ya maneno na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, kuhusu madai waliyoyatoa kuwa
anawindwa kuuawa, mwishoni mwa wiki iliyopita, walijitokeza katika ofisi za
Mtanzania Jumatano na kufunua siri na matukio ya utesaji raia na mauaji ya
kinyama ambayo yamekuwa yakitokea kwa nyakati tofauti kwenye shughuli za
kisiasa hapa nchini.
Wanasiasa hao, Juliana
Shonza na Mtela Mwampamba, ambao wamefanya mahojiano ya ana kwa ana na gazeti
hili, walisema madai waliyoyatoa awali kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.
Willbrod Slaa, alitajwa na kada wa chama hicho, Ben Saanane, kuwa alimtuma
amuwekee sumu Zitto kwa lengo la kumuua ni ya kweli kwa sababu walimkamata
akiwa nayo na alikiri jambo hilo na kumuomba msamaha Zitto kwa kitendo hicho.
Walidai, mbali na tukio hilo
ambalo baada ya kuliibua limegusa hisia za wengi na kuzua mijadala mikali, yapo
matukio mengine ya mauaji na majaribio ya kuua, ambayo yamekuwa yakiratibiwa na
Chadema kwa lengo la kuwagombanisha wananchi na Serikali.
Shonza na Mwampamba walisema
kuwa wapo tayari kutoa ushuhuda wa matukio hayo mahali popote watakapohitajika
na walipoulizwa ni kwa nini baada ya kubaini kuwepo kwa vitendo hivyo,
hawakutoa taarifa kwa vyombo vya sheria au taasisi za ulinzi na usalama,
walisema mlengwa mkuu katika matukio hayo ambayo yalikuwa yakisababisha madhara
kwa watu wengine hakuwa tayari siri hiyo kuanikwa.
Akizungumza mbele ya jopo la
waandishi wa habari wa gazeti la Mtanzania Jumatano, Shonza alidai kuwa, yeye
na baadhi ya vijana wenzake waliokuwa wakiunda kundi Patriotic Movement,
walimnasa Saanane akiwa na sumu hiyo katika Hotel ya Lunch Time iliyoko Ubungo,
Dar es Salaam, ambao awali alidai kuwa ni dawa ya Panya, lakini alipobanwa
alieleza kuwa ilikuwa sumu ambayo hakuitaja jina na kwamba alipewa na Dk. Slaa
ili amuwekee Zitto kwa sababu alikuwa akimsumbua sana.
Alisema, sumu ingewekwa
kwenye kinywaji cha Zitto akiwa katika kikao hicho, lakini hatua yake ya
kutohudhuria ndiyo iliyomuokoa.
Shonza alisema, baada ya
Saanane kukiri kuwa alitumwa na Dk. Slaa kumuwekea Zitto sumu, walimtaarifu
wakati akiwa Marekani na aliporudi alikutana na kuwataka jambo hilo
wasilifikishe polisi kwa sababu lingekivuruga chama na kwamba kwa sababu
alikwishawajua wabaya wake atajilinda.
Alimtuhumu Zitto kwa kuficha
ukweli na kumwita kiongozi mwoga, huku akimuonya kuwa iwapo ataendelea na tabia
ya kukanusha ukweli atamuumbua hadharani kwa sababu anamjua vizuri.
“Ameongea hayo kwa sababu
ana tabia ya kushindwa kuthibitisha kuwa ana uwezo wa kujiongoza yeye mwenyewe
pamoja na wengine. Mtu wa maslahi Zitto, anatafuta huruma ya Chadema baada ya
kuona amepukutika kisiasa kutokana na kukosa msimamo kiuongozi na hawezi tena
kutetea wanyonge, ni mtu mwoga.
Mnapokuwa kwenye mapambano
yeye yuko tayari kurudi nyuma, lakini huruma hiyo asitegemee kuipata Chadema,
labda akubali kushaurika na kubadilika kama kweli anataka kutetea maslahi ya
wanyonge,” alisema Shonza.
Aidha, Shonza alimshambulia
pia Saanane kwa kudai anakataa ukweli anaojua, kwa sababu tukio la kukamatwa
kwake akiwa na sumu lilitokea akiwa mbele ya zaidi ya mtu mmoja na kusisitiza
kuwa kada huyo wa Chadema anatumika na viongozi wa juu wa chama hicho
kuwashughulikia baadhi ya wanachama wasiotakiwa.
Katika hili, Shonza alidai
zaidi kuwa Saanane ni mtu hatari kwa sababu ndiye aliyeanzisha kundi la PM7,
ambalo lilikuwa na lengo la kumpindua Mbowe kutoka kwenye wadhfa wake wa
uenyekiti, lakini baadaye aliwageuka wenzake na kusababisha kufukuzwa katika
chama.
“Saanane alikuwa anatumika
kutuingiza mkenge. Alianzisha kile alichokiita mapinduzi, Patriotic Movement
(PM7), lengo lilikuwa Pindua Mbowe, sisi hatukujua.
Tulikuwa saba katika PM7, Saanane
alifanikiwa kutuchezea akili na alikuja na 'nick names' (majina bandia) yake.
Mimi akaniita Benanzir Bhuto, Mchange akaitwa Mdude, Mwampamba- Joseph Kony,
Zitto- Dogo kama tulivyozoea kumuita na yeye mwenyewe akajiita Cobra, wapo na
wengine sikumbuki vizuri majina yao hapa.
Sisi vijana wakati mwingine
tunatumika vibaya, sisi hatukujua ana ajenda yake, tulivyoshtuka akatukana na
ndiyo yakatokea hayo yaliyotokea,” anazidi kueleza Shonza.
Mwampamba
Kwa upande wake Mwampamba
ambaye aliandamana na Shonza katika ofisi za Mtanzania Jumatano, alidai
kushangazwa na hatua ya Zitto kukanusha kauli ya Shonza iliyokuwa ikieleza
namna Saanane alivyokamatwa akiwa na sumu aliyokuwa ametumwa kumuwekea Zitto.
Alisisitiza kuwa, Zitto
anajua mipango inayopangwa ndani ya Chadema kwa ajili ya kummaliza na alimtaka
aache tabia ya kufunika kombe ili mwanaharamu apite, kwa sababu inaweza kuwa na
athari mbaya kwake.
“Zitto anajua mpango mzima
wa kutaka kumalizwa kwa sumu na Ben Saanane, baada ya kutumwa na Dk. Slaa kwa
sababu tulimwambia na alithibitisha mwenyewe pale Saanane alipomuomba msamaha,
sisi ndiyo tulimbana Saanane hadi akaeleza ukweli wa mipango yao ya mauaji.
“Leo namshangaa
anavyojikomba eti haamini kuwa anaweza kuuawa na hao jamaa. Lakini kwa Ben
Saanane, namtaka atambue kuwa Ludovick alipokamatwa alikanwa na Dk. Slaa wakati
ndiye alikuwa kijana wake mpenzi, sasa na yeye ipo siku atakimbiwa.
“Zitto anatakiwa aache tabia
ya kufunika funika mambo, ajue nimemwokoa sana katika mambo mengi, mfano mauaji
ya Morogoro yaliyopangwa na Chadema yalimlenga Zitto, alikuwa atolewe kafara.
Yule muuza magazeti aliyepigwa risasi Morogoro akafa, siku hiyo ilikuwa afe
Zitto,” alidai Mwampamba.
Alipoulizwa ni kwanini viongozi
wa Chadema wanataka kumuua Zitto, alisema ni kwa sababu ya uhusiano mbaya baina
yake na vigogo hao ambao chanzo chake ni hatua ya kutaka kugombea urais na
kutomuunga mkono Dk. Slaa katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2010.
“Zitto hana uhusiano mzuri
na viongozi wa juu wa Chadema. Nia yake ya kutaka kugombea urais hawaipendi,
inawaudhi sana na amekuwa akitofautiana nao kwa mambo mengi, anajua kuwa
anawindwa ndiyo maana hata oparesheni za M4C hashiriki.
“Mimi nilikuwa Chadema na
nilikuwa karibu sana na Zitto, najua nini kilikuwa kinaendelea juu yake na
najua baadhi ya mambo ya Chadema. Ninaijua mipango ya mauaji ya Chadema. Zitto
aliwahi kuwekewa sumu Bagamoyo wakati wabunge wa chama hicho walipokuwa kwenye
mkutano wao huko.
“Alinusurika kufa. Alipona
baada ya sumu hiyo kutolewa mwilini mwake. Waliiflashi.” Alidai
Mwampamba.
Alidai kuwa Zitto alipata
kunusurika katika ajali ya gari wakati akitokea Bagamoyo kuelekea Iringa, baada
ya gari alilokuwa akitumia kulegezwa nati zinazofunga tairi. Tukio hilo
lilitokea muda mfupi baada ya Zitto na Mbowe kutupiana maneno makali kwenye
mkutano
Kauli ya Saanane
Akizungumza na Mtanzania
Jumatano jana kupitia simu yake ya kiganjani, Saanane alisema madai
yaliyotolewa na Shonza na Mwampamba dhidi yake siyo ya kweli, kwa sababu
wanayodai kuwa walimkamata akiwa na sumu, hakuwa nao.
Alisema kwa mujibu wa
kumbukumbu zake, siku ya Desemba 5, mwaka jana, alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, akikutana na wanaharakati na baadaye jioni alikwenda harusini.
Hata hivyo, alipoulizwa
iwapo alipata kukutana na Shonza na Mwampamba katika Hotel ya Lunch Time,
Saanane alisema amepata kukutana nao mara kadhaa kwa ajili ya kupanga mikakati
ya PM7, ambayo alishiriki kuianzisha lakini aliachana nao baada ya kubaini
walikuwa wakiitumia kwa malengo mabaya.
Mtanzania Jumatano
lilipombana Saanane aeleze mikakati waliyokuwa wakiipanga yeye na wenzake
katika PM7, alisema ilikuwa ya siri na vikao vyao vilikuwa vya siri kutokana na
hofu ya kufikiriwa vibaya na viongozi wa chama iwapo wangebainika wanajihusisha
na kundi hilo.
Alipoulizwa kama
anafahamiana na Zitto na wapi amekwishakutana naye, alisema anamfahamu na
amekuwa akikutana mara kwa mara huku akishangaa tamko lake kwenye mitandao ya
kijamii lilikokuwa likieleza kuwa, hamfahamu na hata akimuona anaweza kupishana
naye.
Hata hivyo, baadaye Saanane
aliomba anuani ya barua pepe ya Mhariri wa gazeti hili na kumtumia barua ya
kumtaka amuombe radhi kwa kuandika habari ya uongo iliyokuwa ikieleza madai ya
masharika wake wanaomuhusisha na tuhuma za kutumwa kumuwekea sumu Zitto, pasipo
kumtafuta Zitto mwenyewe kuzungumza hata neno moja
Vituko vya Dk. Slaa
Dk. Slaa alipotafutwa kwa
simu yake ya kiganjani na kuulizwa kuhusu madai hayo, alianza kuporomosha
matusi mazito huku akilituhumu gazeti hili kutoa nafasi ya kuandika habari
zinazowagusa viongozi wa Chadema badala ya kuandika habari za maendeleo.
“Sina muda wa kujibu maswali
hayo… hayana msingi…tuhuma hizo hazijadiliwi kwenye magazeti……ni masuala ya
kijinga…pumbavu kabisa. Acheni upumbavu bwana. Nina mambo mengi ya msingi ya
kitaifa ya kushughulikia kuliko haya madai ya kipumbavu.” Aling’aka Dk. Slaa.
Hata gazeti hili lilipomsihi
awe mtulivu ili aweze kutoa ushirikiano, aliendelea kufoka huku akiporomosha
matusi zaidi kabla halijaagana naye na kukata simu.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe simu yake iliita muda wote bila majibu na hata Zitto.
CHANZO:MTANZANIA
GAZETI
0 comments:
Post a Comment