.

.
Tuesday, March 12, 2013

2:32 PM


Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea Jumamosi (Machi 16, 2013) kwa mechi tatu zitakazochezwa katika miji ya Mwanza, Dar es Salaam na Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Toto Africans inayopigana kukwepa kurudi daraja la kwanza itakuwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kutoka Tanga katika mechi itakayochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Vinara wa ligi hiyo Yanga wataumana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa wakati Uwanja wa Manungu utakuwa mwenyeji wa mechi ya Mtibwa Sugar na Coastal Union.
UCHAGUZI TAFCA KUFANYIKA MOROGORO
Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) utafanyika Jumamosi (Machi 16 mwaka huu) mjini Dodoma ambapo wajumbe wanatakiwa kuripoti siku moja kabla ya uchaguzi.
Wagombea waliopitishwa kuwania uongozi na Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA chini ya uenyekiti wa Ramadhan Mambosasa ni Oscar Don Koroso (Mwenyekiti), Lister Manyara (Makamu Mwenyekiti) na Katibu (Michael Bundala).
Wengine ni Gabriel Gunda (Katibu Msaidizi), Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania- TFF (Wilfred Kidao) wakati wagombea ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Jemedali Saidi, George Komba na Magoma Rugora.
KIM KUTAJA KIKOSI CHA KUIKABILI MOROCCO
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Kim Poulsen anatarajia kesho (Machi 13 mwaka huu) kutaja kikosi chake kitakachoivaa Morocco.
Mkutano huo wa Waandishi wa Habari utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Machi 24 mwaka huu.
MECHI YA SIMBA, COASTAL YAINGIZA MIL 37/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Coastal Union iliyochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 36,820,000 kutoka na watazamaji 6,284.
Viingilio katika mechi hiyo namba 138 iliyomalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 8,265,752.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 5,616,610.17.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 4,202,924.97, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 2,521,754.98, Kamati ya Ligi sh. 2,521,754.98, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,260,877.49 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 980,682.49.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

0 comments:

Post a Comment