.

.
Friday, March 22, 2013

11:48 PM

Na Bertha Ismail- Arusha

Imebainika kuwa migomo ya daladala inayotokea mara kwa mara hapa mkoani Arusha inasababishwa na vitendo vya rushwa vilivyoota mizizi baina ya madereva wa daladala hizo na askari wa kikosi cha usalama barabarani hali inayoleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wa kawaida wanaotegemea usafiri huo.

Hayo yamebainika hivi karibuni kwenye mgomo wa madereva wa daladala uliotokea mkoani hapa, ikiwa ni siku chache tu tangu yatokee tena miezi ya katikati ya mwaka jana huku yakihusishwa na siasa ambapo hali hiyo ilisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wa kawaida wanaotegemea usafiri huo wakiwemo wanafunzi.

Aidha katika mgomo wa wiki iliyopita, gazeti hili lilifankiwa kuzungumza na baadhi ya madereva wa kisongo, kwa mrombo na Usa ambao hawakuwa tayari kutajwa majina yao, ambapo walisema kuwa wameamua kugoma kushinikiza jeshi la polisi na serikali kwa ujumla kuchukua hatua juu ya askari wa usalama barabarani ambao wamekuwa wakiwaonea kila kukicha kwa kudai fedha zisizo na sababu.

Walisema kuwa askari hao wa usalama barabarani wamewafanya madereva hao kama chanzo cha mapato yao kwani wamekuwa wakiwatoza fedha kila siku kuanzia 150,000 hadi 300,000 bila hata kosa la kimsingi wala onyo hali ambayo imekuwa ikiwatia hasara katika kazi zao wao na wamiliki wa magari hayo bila askri hao kujali hilo.

Waliongeza kuwa endapo wakikataa kulipa fedha hizo barabarani au hata kutoa rushwa ili kusamehewa, hupelekwa kituo cha polisi kwa ajili ya kwenda kuandikiwa karatasi ya madai (notisification) lakini wafikapo hulazimishwa kuwanunulia askari hao chakula au kifungua kinywa ili kupewa karatasi hiyo,

“Endapo ndugu yangu ukishindwa kuwapa hiyo rushwa wanakukamata na kukupeleka kituo cha polisi kati (central) na ukifika kule hataki tena kuandika hadi ukamnunulie kifungua kinywa kama ni asubuhi ambayo unalazimishwa kununua mayai, kuku, chapatti na chai ya maziwa, au kama ni mchana ukamnunulie chakula wakati wewe tangu asubuhi hata hujala muhogo wa kuchoma licha ya kumnunulia askari na kitambi chake kuku…, hii ni haki?” alisema kwa kuuliza mmoja wa madereva hao.

Mbali na hilo walilalamikia pia ukosefu wa vituo maalum vya kupaki magari pamoja na stendi ya kupakia na kushusha abiria kwani ukosefu wa vituo hivyo vimekuwa kama mradi wa kujipatia fedha kwa askari hao endapo dereva akipaki mahala ambapo siyo kituo.

Aidha baada ya mgomo huo uliodumu kwa takribani masaa tisa (9) kuanzia alfajiri ya tarehe 18 hadi saa saba mchana, mkuu wa wilaya ya Arusha John Mongela alikutana na madereva na wamiliki wa magari hayo na kusikiliza kero zao ambapo aliwaahidi kushughulikia na kuwataka kuendeleza huduma hiyo ya usafiri huku yakiendelea kushughulikiwa.


Pia baada ya hapo Mongela alizungumza na waandishi wa habari na kukiri swala la rushwa kuwa chanzo cha mgomo huo kutokana na malalamiko aliyoyapata kutoka kwa madereva na wamiliki wa magari hayo,

“Ukweli usiopingika ni kuwa ukweli rushwa ndio chanzo cha mgomo huo ingawa kunasababu ndogo ndogo pia zimeingia hapo ndani ikiwemo ukosefu wa vituo, miundombinu ya barabara iboreshwe kwani barabara ni chache ikizingatiwa na ongezeko la  idadi ya watu pia kuwepo na stendi ya kupakia na kushusha abiria” alisema Mongela.

 Mongela aliongeza kwa kusema kuwa “ingawa ni kweli rushwa imesababisa mgogoro huo lakini sio jeshi la polisi zima linahusika bali ni tabia ya askari mmoja mmoja ambapo serikali inafanya uchunguzi wa kuwabaini waliohusika ili sheria ichukue mkondo wake kwani hao niwahalifu kama wahalifu wengine.”

Sanjari na hayo pia watu 20 walikamtwa na jeshi la polisi kwa tuhum za kufanya fujo na kuharibu mali za watu, na pia kuuchochea mgomo huo, ikiwemo kuvunja vioo vya gariaina Toyota hiace lenye namba T. 171 BBE mali ya Edward Clegori, pia wanashikilia gari Nissan Caravan namba T 499 CFV mali ya Gabriel Thomas ambalo lilikuwa likitumika kusambaza vijana waliokuwa wanafanya fujo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha.

0 comments:

Post a Comment