.

.
Wednesday, March 20, 2013

6:41 AM

Dar es Salaam
Polisi wa Kikosi cha Dawa za Kulevya, Kilwa road, Jovin Byabusha mwenye namba E.3907 amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kughushi cheti cha elimu ya sekondari na kukitumia kujiunga polisi.
Akisoma hati ya mashtaka jana, Wakili wa Serikali, Aida Kisumo alidai askari huyo, aliingia na kujiunga polisi na kutambuliwa kwa jina la D, CPL Benson Mbelwa Kagya.
Wakili huyo wa Serikali alidai kuwa  Januari 1991 jijini Dar es Salaam askari huyo alikula njama na kughushi cheti cha elimu ya sekondari namba S.407/78  na kuonyesha kuwa kilikuwa ni halali na kwamba kilitolewa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) wakati akijua kuwa ni uongo.
Alidai kuwa Agosti 20, 1994 mshtakiwa huyo pia alighushi fomu  ya Wizara ya Maji na kuonyesha kuwa ni halali na kwamba ilitolewa na  Rwegarulila Resources Institute namba 874403  na wakati si kweli.
Alidai kuwa mshtakiwa alitumia vyeti hivyo vya kughushi kujiunga na polisi nchini Januari 6, 1991 akijitambulisha kuwa yeye ni Benson Mbelwa Kagya wakati akijua kuwa si kweli. Mshtakiwa alikana shtaka upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu Mkazi,  Emillius Mchauru alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika.

0 comments:

Post a Comment