.

.
Saturday, September 7, 2013

11:13 PM


              
Watahiniwa 3000 wa kujitegemea wako hatarini kutofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutokuwa na taarifa zao za kulipia karo za mtihani huo pamoja na zile za usajili.
Tayari Necta imetuma barua kwa watahin
iwa hao kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani mwaka huu.
Licha ya maelezo hayo ya Necta, taarifa zinaonyesha kuwa watahiniwa hao walishalipa ada za mtihani huo kupitia njia mbalimbali za kielektroniki zilizoainishwa na baraza hilo, ikiwamo benki na kampuni za simu za mkononi.
Watahiniwa walipaswa kulipa Sh35,000 ikiwa ni ada za mtihani huo kupitia wakala mbalimbali walioteuliwa na Necta.
Gazeti hili lilifanikiwa kuona barua ya Necta kwenda kwa mmoja wa wanafunzi waliojisajili kufanya mtihani huo kwa mwaka 2013 ikimweleza kuwa, hataweza tena kufanya mtihani huo kwa kuwa hakulipa karo ya mtihani huo.
Barua hiyo ilieleza kuwa, kumbukumbu za Necta zinaonyesha kuwa wanafunzi hao wamejiandikisha kufanya mtihani, lakini hawajawasilisha fomu za usajili wala kulipa karo za mtihani huo.
“Hivyo kwa barua hii, unafahamishwa kuwa umeondolewa kuwa mtahiniwa mwaka 2013,” ilisema sehemu ya barua hiyo zilizosambazwa kwa watahiniwa hao.
Kutokana na kuwepo hali hiyo, baadhi ya watahiniwa kutoka maeneo mbalimbali nchini, wameanza kufuatilia Necta kujua hatima yao wakiwa na vielelezo vya malipo yao.
Ofisa Habari wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), John Nchimbi alithibitisha kuwa baraza hilo liliandika barua kwenda kwa watahiniwa takriban 3,000 waliokuwa wamejiandikisha kama watahiniwa binafsi na kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani huo kwa mwaka huu.
Alifafanua kuwa, baadhi yao walifika Necta wakiwa na stakabadhi zilizothibitisha kuwa wamelipa karo hiyo na hivyo kurudishwa kwenye kundi la watakaofanya mtihani huo mwaka huu.
“Necta hatupokei fedha moja kwa moja, tuna mawakala, kilichotokea ni kuwa baadhi ya watu walilipa karo za mitihani, lakini kwenye mfumo wetu tulikuwa hatuoni kama walilipa,” alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo watu wote walioandikiwa hizo barua ni wale ambao kwenye mfumo wetu hawaonekani kama wamelipa, lakini wengi wa hawa walikuja na risiti zikionyesha kuwa walikuwa wamelipa na wakarudishwa kwenye mfumo,” alisema.
 
 MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment