.

.
Thursday, September 19, 2013

12:19 AM

Kansela wa zamani wa Ujerumani Willy Brandt na aliyekuwa katibu mkuu wa UN Kurt Waldheim mwaka wa 1973
UJERUMANI leo inauadhimisha mwaka wa 40 tangu ijiunge na Umoja wa Mataifa. Waziri wa mambo ya nje Guido Westerwelle ameahidi Ujerumani itaendelea kutoa mchango wake kwa Umoja wa Mataifa wa kudumisha amani duniani.
Miaka 40 iliyopita nchi mbili za kijerumani, Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujerumani zilijiunga na Umoja wa Mataifa.

Nchi mbili hizo za Kijerumani zilijiunga siku moja na Umoja huo,tarehe kama ya leo. Kila upande ulikuwa na mwakilishi wake kwenye Umoja wa Mataifa, hadi nchi hizo mbili zilipoungana tena.

Akizungumza mjini Berlin katika maadhimisho hayo Waziri wa mambo ya nje Guido Westerwelle amesisitiza umuhimu wa siku ya leo na kueleza kuwa kujiunga kwa Ujerumani na Umoja wa Mataifa, ilikuwa hatua ya kurejea katika jumuiya ya kimataifa.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle

Waziri Westerwelle ameeleza kuwa mchango wa Ujerumani katika juhudi za Umoja wa Mataifa ni nyanja mojawapo ya sera ya msingi ya mambo ya nje ya Ujerumani.

Waziri huyo amesisitiza kuwa ni kwa njia ya Umoja wa Mataifa tu kwamba itawezekana kudumisha amani, usalama na kuleta maendeleo duniani.

Wakati huo huo Waziri Westerwelle ametoa mwito wa kuleta mageuzi katika UN.

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani ameeleza madhali taasisi ya Umoja wa Mataifa ipo mstari wa mbele katika utatuzi ya masuala ya kimataifa, taasisi hiyo inapaswa kujigeuza ili iyakidhi mahitaji ya sasa.

Umoja wa Mataifa unapaswa kuwa tayari kufanya mageuzi

Waziri Guido Westerwelle amesema Umoja wa Mataifa unapswa kuwa tayari kufanya mageuzi la sivyo utayapoteza mamlaka yake. Kwa mara nyingine Waziri Westerwelle ameutumia wasaa wa maadhimisho ya mwaka wa 40 ya uanachama wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa kuwasilisha ombi la nchi yake kuwa mwakilishi wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Nembo ya Umoja wa Mataifa

Ujerumani imefanya kazi nzuri kwenye Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka 40 ya uanachama wake. Hayo ameyasema mtaalamu wa masuala ya kisiasa Thomas Weiss kutoka taasisi ya Marekani ya New York Ralph Bunch, ya mausuala ya kimataifa.

Hata hivyo bwana Weiss ambae pia ni mtaalamu wa masuala ya Umoja wa Mataifa ameitaka Ujerumani itoe mchango zaidi katika harakati za Umoja wa Mataifa. Amesema wengi wangependelea kuiona Ujerumani ikishiriki katika majukumu ya kijeshi ya Umoja wa Mataifa. Amesema mshiriki muhimu katika siasa za dunia anapaswa kuyatimiza majukumu ya Umoja wa Mataifa kiuchumi na kijeshi kadhalika.

Ban Ki Moon asema Ujerumani ni mwanachama muhimu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema Ujerumani ni miongoni mwa wanachama muhimu katika jumuiya hiyo.

Katibu mkuu Ban amefahamisha kwamba Ujerumani inashika namba ya tatu katika ukubwa wa michango ya fedha inayotolewa na nchi wanachama kwa ajili ya Umoja wa Mataifa.Katibu Mkuu amesema jumuiya ya kimataifa inaitegemea Ujerumani.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon

Licha ya mchango mkubwa wa fedha unaotolewa na Ujerumani, nchi hiyo haina matumaini makubwa ya kuwa mwanachama wa kudumu kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Wataalamu wa masuala ya Umoja wa Mataifa wanahoji kwamba hali hiyo halisi inatokana na ukweli kwamba, Umoja wa Mataifa utahitaji ufanyiwe mageuzi ili kuweza kuyatekeleza malengo ya nchi fulani. DW

Na jumamtanda

0 comments:

Post a Comment