SHIRIKA na Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) linapoteza zaidi ya
sh bilioni mbili kwa mwaka kutokana na wizi wa mafuta ya transfoma na
uharibifu wa miundombinu ya umeme.
Aidha, Mkoa wa Arusha unaongoza kwa matukio ya uharibifu huo, ukiwamo
wizi wa nyaya za shaba za hasara ya zaidi ya sh milioni 800, ukifuatiwa
na Kilimanjaro zaidi ya sh milioni 400 na Tanga.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Felchesmi Mramba, alieleza hayo jana
wakati akikagua kituo kidogo cha kisasa cha kusambaza umeme
kinachojengwa kwa zaidi ya sh bilioni 11.4 karibu na Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Aliwaomba wananchi kushiriki kikamilifu kuwafichua watu hao wanaolisababishia hasara taifa na kukwamisha juhudi za TANESCO.
Mramba alisema kuwa wanafikiria kukabiliana na wizi wa mafuta kwa
kutumia transfoma zisizotumia mafuta, lakini wamekuwa wakikwama kufanya
hivyo kutokana na gharama ya transfoma hizo kuwa ghali mara tatu ya bei
ya hizi.
Alisema kuwa asilimia 20 ya umeme unapotea kabla ya kumfikia mteja
ambapo tatizo hilo husababishwa na masuala ya kiufundi na yasiyo ya
kiufundi.
Akizungumzia kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha 40 mega voltage
amperes (MVA), alisema kuwa kiko kwenye hatua za mwisho kukamilika na
kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema kuwa kituo hicho kitasaidia kumaliza tatizo la umeme kwenye
mikoa ya Arusha na sehemu za Kilimanjaro na Manyara, ambayo wakati wa
jioni hukabiliwa na tatizo la kuwa na umeme mdogo.
Naye Meneja wa Arusha, Genes Kakore, alitaja maeneo yatakayonufaika na
umeme huo kuwa ni Bomang’ombe, Mirerani, KIA, USA-River na Chuo Kikuu
cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela.
|
0 comments:
Post a Comment