Na Bertha Ismail.
Ikiwa ni siku chache tangu taarifa zizagae juu ya mtalii raia wa Marekani
kuuawa na kundi la Tembo katika hifadhi ya Tarangire, TANAPA wamekanusha vikali
taarifa hizo za mtalii huyo kufia katika hifadhi zao.
Akikanusha taarifa hizo, Meneja uhusiano wa Tanapa, Paschal Shelutete,
alisema kuwa eneo alilokuwa mgeni huyo ni nje ya hifadhi yao ambapo waliwaona
kundi hilo la tembo na kutaka kuwapiga picha ndipo Tembo hao kuwageukia ambapo watalii hao walianza kukimbia ndipo marehem
alipoanguka kwenye tope ambapo Tembo hao walipita juu yake.
“Tukio la mgeni husika lilitokea nje ya hifadhi ya Tarangire katika
kijiji cha Kakoi kambi ya Tarangire River Camp, wakiwa wanafanya utalii wa
kutembea kwa miguu na siyo amefia katika hifadhi zetu kama baadhi ya watu
wanavyodai.”
“Aidha Baada
ya kuvamiwa na kuumizwa, mgeni huyu alifikishwa katika zahanati ya Tarangire na
watumishi wa kambi aliyofikia ambayo iko nje ya hifadhi kwa ajili ya matibabu
ya huduma ya kwanza ambapo alifariki,” alisema Shelutete.
Aidha
taarifa ya TANAPA imekuja baada ya hivi karibuni mtalii mmoja raia wa Marekani,
Thomas Macfee (58), kuuawa na kundi la tembo wakati akiwa kwenye kambi ya Kakoi
Tarangire eneo linalodaiwa kuwa ni mapito ya asili ya wanyama hao lililoko
ndani ya hifadhi ya Tarangire.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Musa Marambo, alipokuwa akitoa
taarifa yake kwa waandishi wa habari hivi karibuni, alisema kuwa tukio hilo
limetokea Agost 30 majira ya saa 2:30
asubuhi baada ya mtalii huyo akiwa na wenzake watano ambao majina yao
hayakupatikana kwa haraka kujaribu
kupiga picha kundi kubwa la tembo lililokuwa likipita karibu na eneo la hifadhi
walilokuwa.
Alisema kuwa wakiwa kwenye harakati za kupiga picha, ghafla tembo hao
walibadili uelekeo na kuanza kuwafuata ndipo wakaanza kukimbia ambapo kwa
bahati mbaya marehem (Macfee) alinasa kwenye dimbwi la matope.
“Baada ya kunasa kwenye matope alishindwa kutoka ndipo tembo wale wakaanza
kumpitia juu na baada ya tembo hao kuvuka
wenzake walimfuata na kumchukua
na kumuwahisha kwenye zahanati ya hifadhi ya taifa ya Tarangire ndipo
akafariki,” alisema Marambo.
Alisema kuwa baada ya kufariki alipelekwa kuhifadhiwa kwenye hospitali ya
Selian jijini Arusha ambapo ubalozi wa Marekani ulimchukua kwa ajili ya
taratibu za mazishi nchini marekani.
0 comments:
Post a Comment