WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema serikali inashughulikia
maombi ya mwekezaji kwenye kinu cha kusaga na kukoboa nafaka cha Arusha
(NMC), Kampuni ya Monaban ya kuomba kuongezewa mkataba au kuuziwa
kiwanda hicho.
Aidha, alimpa pole kwa madai aliyomweleza ya kupata usumbufu kutoka
kwa watendaji wa serikali ambao walifikia kuzima mashine wakati akiwa
anaendelea na usagaji wa nafaka jambo lililosababisha bidhaa hizo
kuharibika.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi baada ya kutembelea kiwanda hicho na
kujionea shughuli za ukoboaji na usagaji wa mahindi na ngano zilivyokuwa
zikiendelea pamoja na kuona ghala la uhifadhi wa bidhaa hizo.
“Nimeona unasononeka na kuumizwa sana na uamuzi wa vinu vingine kuuzwa
na hiki hakikuuzwa, uamuzi ulifikiwa baada ya kuunda bodi ya nafaka
na mazao tukaona hiki na kile cha Iringa tusiviuze viendelee kusimamiwa
na bodi hii.
“Nimeona umewekeza, umefunga mashine mpya, lakini ombi lake Bwana
Molel, apewe kipindi kirefu zaidi au auziwe hiki kiwanda, tumeshaongea
na watu wa kilimo ili watazame na sisi tutaangalia,” alisema.
Pinda aliongeza kuwa huo ndio mchango wa serikali kwenye uwekezaji,
japo wakati mwingine wakiwekeza kwenye mali za umma wale wanaowekwa
wasimamie wanaziua zaidi.
Alipongeza jitihada za Kampuni ya Monaban katika kukifufua kiwanda
hicho sanjari na kushiriki ipasavyo katika kununua mahindi ya wakulima
mpaka ngazi wa chini vijijini, ambapo ameuza mahindi tani 7,600 kwa
wakala wa ghala la chakula la taifa Kanda ya Kaskazini kwa msimu huu wa
kilimo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Monaban, Philip Mollel, alisema kuwa
mwaka 2007 aliingia mkataba wa miaka 15 wa kufufua kinu cha ngano
kilichokuwa kimekufa kwa zaidi ya miaka 10 na kukarabati kinu cha
mahindi ambapo ametumia zaidi ya sh bilioni 6.2 kufanya kazi hiyo.
“Mkataba nilioingia ni wa kufufua, kukarabati, kuendesha na kuzalisha
unga wa ngano na mahindi hapa NMC Arusha kwa miaka 15, ambapo baada ya
kipindi hicho kampuni yetu inaweza kuingia mkataba mwingine,” alisema.
Hata hivyo alisema kuwa kampuni yake inashindwa kufanya
maboresho zaidi, ikiwamo kufunga mitambo mikubwa zaidi, kuweka lami eneo
la ndani ya kiwanda na kujenga uzio imara wa matofali ya saruji
kuzunguka kiwanda hicho kutokana na kukosa ushirikiano kutoka
serikalini.
Hali hiyo alidai inasababishwa na urasimu anaofanyiwa na Shirika Hodhi
la Mitaji (CHC) ambalo hutumia waraka namba 40 wa serikali kumzuia
asinunue kiwanda hicho wakati waliuza viwanda vingine kwa
wafanyabiashara wenye asili ya Asia baada ya waraka huo kuwa umetolewa.
“Hivi majuzi Agosti 31, mwaka huu CHC bila kunipa taarifa huku wakijua
nimewekeza walikuja kiwandani kwa lengo la kukabidhi kiwanda kwa bodi
ya nafaka na mazao mchanganyiko.
“Walifanya hujuma ya kuzima mashine bila taarifa wala ridhaa yangu.
Mpaka sasa sijaelewa lengo lilikuwa ni nini. Uzimaji huo uliisababishia
Monaban hasara kubwa sana hasa ukizingatia kuwa tani 120 za ngano na 60
za mahindi zote kwa pamoja zilikuwa tayari kwenye mfumo na mchakato wa
uzalishaji hivyo nafaka hizo ziliharibika,” alisema
0 comments:
Post a Comment