.

.
Tuesday, December 3, 2013

 Dalili za amani na usalama Mkoa wa Arusha zimeanza kuonekana mapema baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwakutanisha viongozi mbalimbali vya vyama vya siasa, dini na wabunge wa vyama tofauti kujadili changamoto kuu katika suala la amani.
Katika kipindi cha hivi karibuni, Arusha umekumbwa na vurugu za hapa na pale hali iliyosababisha baadhi kupoteza maisha katika matukio tofauti likiwamo bomu lililolipuka katika mkutano wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa Chadema eneo la Soweto na kuua watu 4 na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa.
Katika mkutano uliofanyika jana, ilitolewa kauli moja ya kuitisha mkutano mkubwa wa amani utakaofanyika Desemba 6 mwaka huu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Mkutano huo utawashirikisha wafuasi kutoka vyama mbalimbali vya siasa, dini tofauti na wale wasio na vyama ambapo katika makubaliano yaliyoafikiwa kuelekea katika mkutano huo mojawapo ni washiriki kutovaa sare za vyama vyao.
Akifungua mkutano huo, Msajili Francis Mutungi alisema kuwa lengo la ofisi yake kuwakutanisha wadau hao ni kutafuta amani mkoani Arusha.
Alisema kuwa hakuna mtu anayestahili kuipuuza amani katika Mkoa wa Arusha, ambao unachangia pato kubwa la taifa hususan katika sekta ya utalii.
Mutungi alisema wakazi wa Arusha wanapaswa kuzingatia amani katikati ya udini na ukabila. “Ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anasaidia kuleta amani katika eneo lake kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na jeshi la polisi,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema kuwa changamoto kubwa katika mkoa wake ni suala la amani.

0 comments:

Post a Comment