.

.
Friday, December 6, 2013

Mkutano wa chadema ukihutubiwa na mwk wa chama hicho Mbowe, picha na  maktaba yetu ya BERTHA BLOG
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)
CHADEMA MKOA WA ARUSHA
H/SE NO 8 NHC STREET
NGARENARO
Kumb. Na: CDM/MKA/MV.1/5 5/12/2013
MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA
P.O.BOX
DAR ES SALAAM.

YAH: MKUTANO WA HADHARA WA WADAU WA AMANI ARUSHA .
Husika na kichwa cha habari

Tafadhali rejea maazimio ya kikao kilichofanyika ofisini kwako,na baadae kikao cha viongozi wa vyama vya siasa,na viongozi wa dini na wabunge wa mkoa wa Arusha Naura Spring,pamoja na mambo mengine tulikubaliana kuwepo kwa mkutano wa hadhara wa vyama vyote December 6 uwanja wa Sheih Amri Abeid Arusha.
Aidha tulikubaliana kimsingi kuwa lengo la mkutano sio mwafaka baina yetu sisi CHADEMA na ccm au na chama chochote cha siasa,bali ni kutafuta namna bora ya kufanya siasa za KIUNGWANA zitakazodumisha amani,kama ambavyo imekuwa ni kilio cha CHADEMA muda mrefu.Hata hivyo kwenye vikao vyote tulieleza kuwa chanzo cha kutokuwepo kwa amani Arusha ni UCHAGUZI BATILI wa MEYA Arusha.
Kwa masikitiko makubwa tunapenda kukufahamisha kuwa kumekuwepo na upotoshwaji wa makusudi wa lengo la mkutano huu, upotoshwaji unaofanywa na vyombo vya habari hasa vinavyomilikiwa na ccm kama gazeti la uhuru lilivyonukuliwa kwa kichwa cha habari “CHADEMA maji shingo, yatafuta suluhu na ccm”, napia mtangazaji aliyekuwa akitangaza kwa kipaza sauti kufanya mualiko kwa wakazi wa arusha kuja kwenye mkutano huu, amenukuliwa akitangaza kuwa “December 6 kutakuwa na mwafaka kati ya CHADEMA na CCM”. Ni wazi kabisa kuwa kwa makusudi CCM wameamua kupotosha kabisa lengo la mkutano huo, na hivyo kuharibu nia njema ya ofisi ya msajili, kwa sababu hizo tunapendekeza mkutano huu usogezwe mbele na pia tunakufahamisha kuwa HATUTASHIRIKI kwenye mkutano wa tarehe 6 Desemba mpaka jambo hili litakapopanuliwa ili kuchukua sura ya ushirikishwaji kitaifa na pia kuushusha mjadala huu kwa wananchi wenyewe kwa kuzingatia sababu zifuatazo;
1 . Upotoshwaji ambao umeshafanywa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na ccm pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali wa ccm,unaondoa dhamira njema ya ofisi yako na wadau wengine wa amani,hivyo kufanya juhudi zote hizi kuwa BURE, rejea gazeti la uhuru hapo juu pamoja na Mtangazaji aliyepita kutangaza kuwa December 6 ni siku ya mwafaka kati ya CCM na CHADEMA
2 .KAULI YA MH WAZIRI MKUU PINDA,kuwa wapigwe tu, imeendelea kuleta madhara makubwa sana kwa wananchi hasa wanachama wetu wa mkoa wa Arusha , hata hivyo CHADEMA inaona umuhimu wa Viongozi wa Dini kuwa jasiri na kukemea kauli kama hizi kwa nguvu zote . Kwa hivyo nia njema ya msajili inakosa mamlaka ya kutetea Amani inayoisema wakati Watawala wakubwa wametoa maelekezo ya unyanyasaji na ukatili mkubwa kwa Jamii .
3 . WELEDI WA JESHI LA POLISI , Jeshi la Polisi ambalo Viongozi wake walikuwepo katika vikao vya majadiliano ya mkutano unaopaswa kufanyika Ijumaa wameendelea kutumika kisiasa na siku ya jana tarehe nne wamethibitisha kwa kutoa taarifa chafu na mbaya kuhusu tukio la moto ambalo limetokea hivi karibuni kwa kuhusisha tukio hilo na Chadema jambo ambalo limechafua sura nzima ya malengo muhimu ya Msajili wa Vyama vya Siasa . Hata matamko haya yanakwenda na propaganda chafu ambazo zimefanywa huko nyuma haswa pale tulipoandama kwa kufuata taratibu na tulipopigwa bomu katika Mkutano wa Soweto. CHADEMA tunaushahidi wa Polisi kuhusika na tukio hilo na CHADEMA tuliomba Mh Raisi aunde tume Huru ya Kimahakama ili kupeleka ushahidi wetu huko lakini mpaka leo CHADEMA wameendelea kupuuzwa huku Polisi wakiendelea kukamata watu na kuwatesa na kuwalazimisha kuwataja Viongozi wa CHAMA kama wahusika wa tukio la Soweto .
4 . UCHAGUZI WA MEYA WA ARUSHA MJINI . Mfarakano wa CCM na CHADEMA ulianza pale ambapo Meya alichaguliwa pasipo kufuata taratibu na kanuni , kwa hiyo kuzungumzia Amani bila kutafakari mgogoro huu ni sawa na kufikiri kwamba dhambi inaishia kwa kukaa muda mrefu na sio kutubu . Hivyo ni muhimu mambo haya yakaingia kwenye mjadala huu kama kweli Msajili wa Vyama vya Siasa anatafuta suluhu ya hakika na kweli. Suala la umeya tumelitafakari sana, dhamira zetu njema zimekataa kabisa kukubaliana na uhuni huu wa ukiukwaji na uvunjwaji wa kanuni uliofanyika. Msimamo wetu ni kuwa hatumtambui meya wa ccm Gaudence Lyimo na hivyo tunasisitiza meza ya majadiliano ili kumaliza mgogoro huu. Tunashangazwa na kusikitishwa na unafiki wa kutaka amani kunakofanywa na CCM na serikali yake kwa kuigiza wanahubiri amani wakati ndio wavunjaji wakubwa wa kanuni, haki na utu.
5 . UKABILA NA UDINI . CCM kwanza ikemee kwa nguvu na Serikali kufungua mashitaka dhidi mkutano uliofanywa na kuratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Naibu Waziri Ardhi Mh Ole Medeye eneo la Chuo cha Ufundi Arusha ukiwa na Ajenda ya Siasa za ukabila , Mkutano huu ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Ardhi na ajenda hiyo chafu iliitimishwa mbele ya Naibu Waziri kwa kutoa kauli kwa kuwaondoa na kuwaua Watu wasio Wamasai au Waarusha katika Mji wa Arusha , pamoja na kuwepo na ushahidi wa video lakini mpaka leo hakuna hatua za kisheria zimechukuliwa .
Hitimisho . CHADEMA inatambua Umuhimu wa Amani na Maendeleo lakini CHADEMA inaamini kuwa Amani ni tunda la Haki , hivyo basi ni matumaini yetu kama CHAMA na kumuomba msajili wa Vyama vya Siasa atazame kwa makini ni wapi Taifa limekwenda kombo na kuchochea hali hii ya Taifa kuwa ilivyo sasa kwani Serikali imekuwa kwa makusudi sana ikipuuza Haki na Utu na kuleta mashaka makubwa katika Taifa letu .
Kwa msingi huu tunamuomba Msajili wa Vyama vya Siasa Judge Francis Mtungi aendelee na jitihada zake hizi nzuri lakini kuomba ofisi yake ipanue mjadala huu na kuhusisha Viongozi wakubwa wa Kitaifa na Serikali ili kutoa fursa ya majadiliano ambayo italeta afya kubwa katika Taifa letu . Hata hivyo kuhusu Mkutano ambao ulikuwa ufanyike kesho tarehe 6 Desemba , CHADEMA Mkoa wa Arusha inaomba ofisi ya msajili ipeleke mkutano huu tarehe za mbele ili kutoa fursa pana ya ndani ya kujadili mambo haya ya msingi ambayo yanaonekana kuwa na sura nyingi zinazoleta mgongamo mkubwa wa kifikra .
“ Na yeyote anayetaja Amani kinywani mwake na awe wa kwanza kutenda Haki “
Nakutakia kazi njema .

KATIBU MKOA ARUSHA .
Amani Golugwa.
5 Desemba 2013
Nakala : Katibu Mkuu(T) - CHADEMA
Viongozi wa Dini na Madhehebu yote Mkoa Arusha .
Wenyeviti Vyama vya Siasa Mkoa .
Idara ya Usalama wa Taifa Mkoa .

0 comments:

Post a Comment