.

.
Sunday, December 29, 2013

8:55 PM

Rais Kikwete anafanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ikiwa imepita miezi 18 tangu alipowang’oa mawaziri wanane kutokana na tuhuma mbalimbali.   

DAR ES SALAAM. 
RAIS Jakaya Kikwete anatarajia kuipanga upya safu ya Baraza lake la Mawaziri wakati wowote, huku baadhi ya naibu mawaziri wakipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mawaziri kamili.


Hatua hiyo inatokana  na uamuzi wake wa  kutengua uteuzi wa mawaziri wanne alioufanya siku tisa zilizopita, mawaziri hao walishutumiwa kushindwa kuwajibika  katika utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Ripoti ya kamati ndogo ya  Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyoundwa kuchunguza operesheni hiyo, ilieleza kuwa athari zilizotokana na operesheni hiyo zilisababishwa na wizara nne zilizokuwa zikiongozwa na mawaziri hao.

Waliong’olewa katika sakata hilo ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David.

Rais Kikwete anafanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ikiwa imepita miezi 18 tangu alipowang’oa mawaziri wanane kutokana na tuhuma mbalimbali.

Historia inaonyesha kuwa Rais Kikwete amekuwa na utaratibu wa kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua, huku akiwapandisha naibu mawaziri kuwa mawaziri.

Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa marekebisho inampa mamlaka Rais kuwateua wabunge 10, mpaka sasa ameshawateua wanane na kubakiza nafasi mbili pekee.
Kati ya wabunge wanane walioteuliwa na Rais Kikwete, watano walipewa wizara za kuziongoza.

Wabunge hao na wizara zao kwenye mabano ni Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).

Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini), na Saada Mkuya na Janet Mbene (wote ni Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha).

Kutokana na utamaduni huo, Dk Asha-Rose Migiro anapewa nafasi kubwa ya kuingia kwenye baraza jipya la mawaziri, kwani naye hivi karibuni ameteuliwa kuwa mbunge.

Wabunge ambao wameteuliwa na Rais lakini hakuwapa uwaziri mpaka sasa ni Zakia Meghji, James Mbatia na Dk Asha-Rose Migiro.
                                                                                               MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment