.

.
Tuesday, December 3, 2013

1:30 PM
Watalii watatembela  mbuga kuangalia miti baada ya kuona picha hii ya tembo makumbusho? embu ona mbuga inavyopendeza kwa kuwa na wanyama hawa jamani.

Na Bertha Ismail

TEMBO waliopo nchini wanaokadiriwa kuwa sio zaidi ya 70,000  watakuwa wamefutika katika uso wa dunia nchini kwetu miaka michache ijao endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kukabiliana na majangili.

Katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo kusini mwa Tanzania ambayo ni Hifadhi ya Taifa kubwa kuliko zote nchini yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,226 ina tembo zaidi ya 30,000 ,utafiti umebaini kuwa majangili yamekuwa yanawauwa tembo hao kwa kasi hali  inayotishia uwepo wa wanyama hao ndani ya hifadhi hiyo.

Kwa uchunguzi uliobainika, baadhi ya majangili  ambao walikamatwa katika hifadhi hiyo walikutwa wakitumia silaha za kisasa zikiwemo zile ambao zilitumika katika vita ya Idd Amini wa Uganda kati ya mwaka 1978 hadi 1979.


Utafiti ambao ulifanywa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwaka 1985 ulibaini kuwa vitendo vya ujangili ambavyo vilikuwa vinafanywa na jamii inayozunguka hifadhi hiyo vilisababisha idadi ya tembo katika hifadhi hiyo kupungua kutoka tembo 2500 hadi kufikia tembo wasiozidi 500 .

Taarifa za  (TANAPA) zinabainisha kuwa utafiti ambao ulifanywa mwaka 2011 unaonyesha kuwa ujangili unasababisha katika Tanzania tembo zaidi ya 30 kufa kila siku sawa na tembo 850 kwa mwezi na tembo zaidi ya 10,000 wanauwawa kila mwaka hali inayohatarisha wanyama hao kufutika katika Tanzania.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika pori la akiba la Selous hadi kufikia mwaka 2007 kulikuwa na tembo zaidi ya 70,000 hata hivyo idadi ya tembo katika pori hilo imeshuka kutokana na kukithiri kwa ujangili hadi kufikia tembo 43,000 mwaka 2009 ambapo hivi sasa  inakadiriwa huenda idadi ya tembo katika pori hilo imeshuka na kufikia 30,000 tu.

Shehena ya meno ya tembo iliyokamatwa nchini China mwaka 2012 kutoka hapa nchini ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani milioni moja na nusu. Wiki mbili kabla ya hapo takribani tani nne za meno ya Tembo zilikamatwa huko huko HongKong katika nchi ya China.

Matukio haya mawili ya shehena za meno ya tembo ni sawa na Tembo 900 waliouwawa.Hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa ujangili umeshamiri kwa kasi ya kutisha na kuhatarisha maisha ya wanyamapori hususani tembo.

Takwimu za Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii zinaonyesha kuwa mwaka 2010 hapa nchini jumla ya Tembo 10,000 waliuwawa, takwimu hizo ni sawa na Tembo 37 waliuwawa kila siku.

Kulingana na takwimu hizo hali ilikuwa mbaya zaidi mwaka 2012 ambapo jumla ya Tembo 23,000 waliuwawa sawa na wastani wa Tembo 63 kila siku, kutokana na kasi hii ya ujangili, ifikapo mwaka 2018 inakadiriwa Tanzania haitakuwa na Tembo hata mmoja.

Mimi kama mtanzania hali hii inanitisha sana ukizingatia umuhimu wa wanyama hao hasa katika hifadhi zetu, ambapo mbali na kuongeza pato la taifa na kuingiza fedha za kigeni pia inaipatia nchi yetu heshima ya utalii.
Hakuna hifadhi ya aina yoyote duniani watu hutembelea kuona msitu, panya pori (buku) wala mende bali simba, chui, tembo, mbogo n.k.


Pamoja na hatari hiyo ya kuwapoteza wanyama hawa, mimi sijawahi kusikia adhabu wanayopewa hawa wanaokamtwa na meno ya tembo kila kukicha na kama huwa napitiwa na taarifa hizo naomba nikumbushwe kwani tumekuwa nimekuwa nikisikia wakikamatwa lakini adhabu yao siijui.


Ninachojiuliza, je siku tembo hawa wakipotea wao na kizazi chote watalii wataendelea kuitaja nchi yetu kwa kuja kuangalia picha za historia za wanyama hao maana nimehudhuria mikutano mingi ya kimataifa ambapo wakimaliza mkutano siku ya mwisho hupendekeza kwenda mbuga za wanyama kabla ya kurudi makwao.

0 comments:

Post a Comment