.

.
Sunday, December 22, 2013

2:44 AM
                                                                  
Thobias Andengenye akitoa taarifa kwa waandishi wa habari 2010 alipokuwa kamanda wa polisi mkoa wa Arusha


MSTARI wa kumpata mrithi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema, umechorwa chini ya maofisa watatu wa jeshi hilo, Raia Mwema limeelezwa.




Vyanzo vilivyozungumza na gazeti hili kutoka ndani ya Jeshi la Polisi na serikalini vimeeleza kwamba tayari majina hayo matatu yamefikishwa mezani kwa Rais Jakaya Kikwete tayari kwa uamuzi.



Maofisa wanaotajwa kuweza kumrithi IGP Mwema ni Kamishina Msaidizi wa Polisi, Thobias Andengenye wa Makao Makuu ya Polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ernest Mangu na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani.



IGP Mwema anatarajiwa kustaafu rasmi mwisho wa mwaka huu, ingawa alitakiwa kustaafu tangu Juni kwa mujibu wa sheria, lakini akaongezewa muda wa miezi sita na Rais Kikwete kutokana na changamoto mbalimbali zilizokuwa zikilikabili jeshi hilo.

Uwezo na upungufu kwa kila mmoja

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Saidi Mwema akimvisha cheo kipya cha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Polis, Thobias Andengenye ambaye hapo awali alikua Kamisha Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP). Hafla hiyo fupi iliyofanyika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Picha ya Maktaba. 

Duru mbalimbali zilizozungumza na askari zimembainisha kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa kushika nafasi hiyo kutokana na msimamo wake usioyumba, weledi na usomi wake. 



Andengenye alijiunga katika Jeshi la Polisi akitokea masomoni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikopata shahada yake ya kwanza katika Utawala na Uhusiano wa Kimataifa. 



Amefanya kazi katika mikoa mbalimbali kwa nafasi mbalimbali na ingawa ana umri wa miaka 49, tayari amepitia changamoto nyingi na anatajwa kulifahamu Jeshi la Polisi vizuri.



Faida
Mwaka juzi, Andengenye alipelekwa mafunzoni katika chuo maarufu cha Bramshill nchini Uingereza alikosomea uongozi. 



Hiki ni chuo ambacho wakuu wawili waliopita wa jeshi hilo, Mwema na Omar Mahita, walipita kabla ya kuupata wadhifa huo. Kamanda huyu ambaye anashikilia wadhifa wa Mkuu wa Rasilimali Watu wa Jeshi hilo ana faida nyingine ya kuwahi kuwa msaidizi (Aide-de-Camp) wa IGP Mahita, nafasi iliyompa fursa ya kulifahamu vema jeshi hilo na siasa zake. 


Andengenye aliyewahi pia kuwa Kamanda wa Polisi wa mikoa ya Morogoro na Arusha, anatajwa kuwa mtu asiye na majivuno, anayezungumza vizuri na kila mtu. 



Udhaifu
Kihistoria, wakuu wote wa polisi waliopita walianzia mafunzo yao katika Chuo Kikuu cha Polisi Moshi (CCP). Maana yake wengi wao walianzia ngazi za chini kabisa na kupanda taratibu hadi kufikia wadhifa wa juu kabisa. 



Kuanzia ngazi za chini maana yake ni kuwa walipangiwa zamu za lindo, waliongoza magari, waliishi katika barracks (kambi) na kujifunza kila kitu kuanzia kunyoosha nguo, kutandika vitanda, kuwa na nidhamu ya kazi. 



“Wakija kuwa ma-IGP maana yake walikuwa wanajua kila kitu kuhusu jeshi maana wamepitia kila kitu. Hii ndiyo faida ambayo IGP aliyeanzia chini anayo,” kilisema chanzo kimoja cha gazeti hili ambacho hatutakitaja jina kwa sababu za wazi.



Kutokana na elimu yake, Andengenye alipata mafunzo yake ya uaskari katika chuo cha maofisa wa polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam na hakuwahi kupita CCP. 



Hiki ndicho kinachoelezwa kuwa kigingi kikuu cha Andengenye.

ACP Diwani.

Askari huyu ambaye ni msomi mwenye elimu ya shahada ya kwanza ya sheria amejijengea heshima kwa jinsi alivyoutuliza Mkoa wa Mbeya unaoelezwa kuwa miongoni mwa mikoa iliyo migumu kuiongoza.

Anasifika pia kwa kutoyumba kwenye msimamo, sifa inayomtofautisha na askari wengi wa kizazi chake ambao ni waoga kwenye masuala ya uamuzi.

Faida
Zaidi ya usomi wake, Diwani alipata pia bahati ya kuwa ADC wa IGP Mahita jambo linalomfanya kuwa na uelewa mpana kuhusu jeshi hilo, ‘siasa’ zake na utendaji wake.

Udhaifu
Kama ilivyo kwa Andengenye, Diwani naye hakupitia CCP jambo linalozua maswali kama yale yaliyopo kwa mwenzake huyo. 



Pia, ingawa wana baadhi ya sifa zinazofanana, Andengenye anamzidi kwa cheo na alimtangulia kuwa ADC wa Mahita na kuwa Kamishina wa Polisi. 



Vyanzo vya Jeshi la Polisi vilivyozungumza na gazeti hili vimesema kwamba kama Andengenye asingekuwepo, Diwani angekuwa na nafasi kubwa.


Kamanda Ernest Mangu akitoa taarifa.

Kamanda huyu wa Mwanza anaheshimika sana ndani ya Jeshi la Polisi. Tangu achukue mikoba iliyoachwa wazi na hayati Liberatus Barlow aliyekuwa akishikilia wadhifa huo na kuuawa kikatili, Mangu amefanya vema. 



Anatajwa kuwa msomi wa shahada ya kwanza katika Sayansi ya Polisi (Police Science) aliyoipata ughaibuni. Anaelezwa kuwa msimamizi mzuri wa misingi ya upolisi kama ilivyoainishwa katika Police General Order (PGO). 



Siku hizi, askari hawafuati misingi ya upolisi kama ilivyo kwenye PGO. Misingi inasema, kwa mfano, askari hatakiwi kuacha lindo hadi mwenzake afike lakini siku hizi askari anaacha silaha lindoni kabla mwenzake hajafika.



“Ni jambo la kawaida siku hizi kuona askari akiingia kazini huku amelewa. Lakini kwenye PGO unaambiwa kabla askari hajaingia lindoni ni lazima akaguliwe lakini hilo halifanyiki siku hizi. Mangu anaweza kusimamia PGO,” kilisema chanzo hicho.



Faida
Katika majina haya matatu, ni Mangu pekee ambaye amepitia CCP kulinganisha na wenzake. Kama atateuliwa kuwa IGP, itakuwa ni kuendeleza utaratibu wa kuwapa nafasi waliopitia katika chuo hicho. 



Udhaifu
Mangu anadaiwa kuandamwa na kashfa za ukabila. Raia Mwema limeambiwa yapo madai kwamba kuna kipindi alipewa nafasi katika makao makuu ya Jeshi la Polisi na aliteua watu wengi kutoka mkoani kwake, Singida, kila fursa ilipojitokeza. 



“Kama kuna kitu ambacho kimemuharibia sifa Mangu ni madai ya kuwa na ukabila. Angekuwa na nafasi isiyo ya kawaida bila ya kashfa. Sasa kama alionyesha makucha yake katika nafasi ya chini, akiwa IGP itakuaje?” kilisema chanzo cha gazeti hili. 



Changamoto za IGP mpya
Ingawa anasifiwa kwa kulipeleka jeshi karibu na wananchi kupitia mfumo wa Polisi Jamii, IGP Mwema analaumiwa kwa kushusha nidhamu ndani ya jeshi. 



Chanzo cha matatizo mengi ya sasa ni ukosefu wa nidhamu na ufuatiliaji. Sare feki na bunduki zinakamatwa hovyo kwa sababu askari hawakaguliwi kama ilivyokuwa zamani. 



“Maadili yakiboreshwa kila kitu kitabadilika. Wanaolinda watafanya kazi zao, wanaofanya doria watafanya kazi yao na wakubwa wataangalia maslahi ya wadogo. Hivi ndivyo polisi wanavyofunzwa,” kilisema chanzo hicho. 



Raia Mwema limeelezwa kwamba kamanda mwenye uelewa mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira ya kisasa ya utandawazi na mihemuko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi atakuwa na nafasi kutokana na changamoto zilizopo sasa. 

http://www.thehabari.com/wp-content/uploads/2013/10/IGP-Said-Mwema-Akikagua-gwaride.jpg
Waliotangulia wadhifa wa IGP
IGP wa kwanza Mtanzania baada ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika ni Elengwa Shaidi. Waliofuata ni Hamza Aziz, Samson Pundugu, Philemon Mgaya, Solomon Liani, Harun Mahundi, Omar Mahita na Saidi Mwema

0 comments:

Post a Comment