.

.
Sunday, January 6, 2013

12:48 PM
JESHI la Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia askari wawili kutoka mkoani Kagera pamoja na raia wawili baada ya kukutwa na vipande 17 vya meno ya tembo.
Akizungunza na Tanzania Daima, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Absalom Mwakyoma, alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa kuamkia jana saa nane katika Kijiji cha Lwamchanga, Tarafa ya Logoro wilayani Serengeti.
Mwakyoma alisema kuwa siku hiyo, askari waliokuwa doria, kwa kushirikiana na askari wa kikosi cha wanyama pori, waliwakamata watu wawili, Boniface Kurwa (31) mkazi wa Geita akiwa na pikipiki yenye namba za usajili T 874 CCC aina ya Sunlg akiwa na mwenzake Nyarata mkazi wa mjini Mugumu ambaye pia alikuwa na pikipiki namba T 834 ZPH aina ya Toyo.
Alisema kuwa baada ya kusimamishwa na askari hao, walitupa pikipiki na kukimbia, lakini Kurwa alikamatwa, na pikipiki zao zilipokaguliwa zilikutwa zimepakia vipande 17 vya meno ya tembo.
Kamanda alisema kwa idadi ya meno hayo, ni sawa na tembo watatu wameuawa na kwamba baada ya kukamatwa, Kurwa alitoa ushirikiano akidai kuwa waliowatuma pembe hizo wapo katika hoteli moja iitwayo Garakisi ya mjini Mugumu.
Aliongeza kuwa walikwenda na kuwakuta askari wawili mmoja mwenye namba E 9172 D/C, Koplo David ambaye ni wa Kituo cha Polisi Biharamulo na F 5553 D/C Jerad wa Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai Bukoba.
“Baada ya kuhojiwa, askari hao walikiri kuwa wamefika huko baada ya kuelekezwa na mtu mmoja aitwaye Boniface Emmanuel maarufu kama Mnyarwanda ambaye ni mkazi wa huko Biharamulo,’’ alisema.
Kamanda alisema kuwa askari hao walikuwa na gari dogo lenye namba za usajili T 403 BTK aina ya Carina mali ya D/C Jerad ambalo pia limeshikiliwa na polisi, huku watuhumiwa wote wakitarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote upelelezi utakapokamilika.
chanzo:Tanzania daima

0 comments:

Post a Comment