.

.
Tuesday, January 29, 2013

11:21 PM
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRD), umedai kupokea kwa mshangao taarifa zilizoandikwa na gazeti la serikali zikisema kuwa Rais Jakaya Kikwete amelizika rasmi gazeti la MwanaHalisi kwa uchochezi.
Kwamba habari hiyo imeupotosha umma kwa kiwango kikubwa, na hivyo wanaitaka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kutoa ufafanuzi, kutokana na kupotoshwa kwa kosa lililosababisha gazeti hilo kufungiwa.
Mtandao huo ambao ni mkusanyiko wa mashirika zaidi ya 60 ya watetezi wa haki za binadamu wakiwamo wanasheria, waandishi na watetezi wengine, ulisema kuwa habari hizo ni za upotoshaji kwa sababu zinamkariri Rais Kikwete akiwa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Kwamba habari iliyochapishwa na gazeti hilo la HabariLeo ilidai kuwa MwanaHalisi lilifungiwa kwa sababu liliandika habari ya uchochezi ikiwataka askari kuasi na kutotii amri.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mratibu wa Mtandao huo, Onesmo Olengurumwa alisema kuwa habari hiyo haikuandikwa na gazeti la MwanaHalisi bali gazeti jingine ambapo tayari watuhumiwa wamefikishwa mahakamani.
“Tunaamini kilichoandikwa na mwandishi wa gazeti hilo ndiyo kauli iliyotolewa na Rais Kikwete kwa sababu habari hiyo imeletwa na mhariri mzoefu na makini, na tunaamini hivyo kwa sababu rais ameitoa kauli hiyo mahali pake, wakati akiwasilisha ripoti ya Tathmini ya Utawala Bora (APRM),” alisema.
Aliongeza kuwa, wanashawishika kuamini kwamba iwapo siku zote Rais Kikwete alikuwa akiamini kuwa MwanaHalisi ndiyo waliochapisha habari inayohusu askari kugoma, basi alipotoshwa tangu mwanzo na hivyo anahitaji kuelimishwa vizuri juu ya suala hilo.
Alisisitiza kuwa, wanaendelea kuamini kuwa MwanaHalisi lilionewa kama sababu zilizosababishwa kufungiwa ni pamoja na zile ambazo gazeti hilo lilimnukuu Rais Kikwete huko Ethiopia.
Katika habari hiyo, Rais Kikwete alikaririwa akisema “...Ndio kuna gazeti moja tumelifungia na kuna watu wanaosema tuliondolee adhabu…tumesema hapana…kutaka Jeshi liasi huu sio uandishi wa habari.”
MwanaHalisi lilifungiwa na serikali Julai 30 mwaka jana, kutokana na habari yake iliyomhusisha ofisa wa Ikulu katika sakata la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, kudaiwa kuwa ni ya uchochezi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers (HHPL) inayochapisha MwanaHalisi, Saed Kubenea, alipoulizwa juu ya kauli ya rais, alisema ameipokea kwa faraja.
“Tuna taarifa za serikali kukamata na kushitaki mwandishi aliyeandika habari ambazo serikali ilisema zinachochea uasi katika majeshi; mhariri wa gazeti lililozichapisha na mwenye mtambo uliochapa gazeti. Lakini hayo yote hayahusu MwanaHalisi,” alisema.
Alisema kuwa kwake si gazeti wala waandishi wa habari wanaotuhumiwa uchochezi wa jeshi. Lakini kama walifungiwa kwa madai hayo, basi sasa rais ameibuka na ukweli ambao utawaweka huru.
chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment