.

.
Sunday, January 20, 2013

12:40 PM
Kiemba, shujaa wa Simba leo

Na Nurat Mahmoud, Muscat
SIMBA SC imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza katika ziara yake ya Oman jioni hii, baada ya kuifunga Ahly Sidab kwenye Uwanja wa Sidab mjini Muscat.
Katika mchezo huo, shujaa wa Simba, alikuwa ni kiungo aliyerudi juu kisoka hivi sasa, Amri Ramadhan Kiemba aliyeifungia timu hiyo bao la ushindi.
Katika mechi hiyo nzuri na ya kusisimua, wenyeji ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kipindi cha kwanza, lililofungwa na kiungo Mbrazil, aitwaye Lopez, kabla ya kiungo wa Simba, Kiggi Makassy kusawazisha kipindi hicho hicho cha kwanza.
Hadi mapumziko, timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1 na leo Simba walicheza soka nzuri mno, huku wachezaji vijana, Miraj Adam, Abdallah Seseme, Haroun Chanongo na Shomari Kapombe waking’ara zaidi.  
Kipindi cha pili, kocha Mfaransa, Patrick Liewig alifanya mabadiliko, akiwaingiza Rashid Ismail, Marcel Kaheza wote waliopandishwa kutoka timu B na Kiemba ambao waliongeza makali ya Mnyama na hatimaye kupata ushindi huo.
Alikuwa ni kiungo wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga SC, Miembeni na Moro United aliyeipatia Simba ushindi wa kwanza katika ziara yake ya Oman kwa kufunga bao safi la ushindi dakika za mwishoni.
Huo ulikuwa mchezo wa tatu kwa Simba katika ziara hiyo, awali ikifungwa 1-0 na U23 ya Oman na baadaye 3-1 na timu ya Jeshi la nchi hiyo, Qaboos, bao la Wekundu hao wa Msimbazi, likifungwa na Haruna Moshi ‘Boban’.   
Huo ulikuwa mchezo wa sita kwa Mfaransa, Liewig kuiongoza Simba tangu aanze kazi mapema mwezi huu, awali akishinda mechi moja, sare mbili na kufungwa mbili.
Aliiongoza Simba SC kuifunga 4-2 Jamhuri, sare ya 1-1 na Tusker FC, 1-1 na Bandari zote katika Kombe la Mapinduzi Zanzibar, kabla ya kufungwa 1-0 na U23 ya Oman na 3-1 dhidi ya Qaboos katika ziara ya Oman.
Simba SC inatarajiwa kurejea nchini Jumatano baada ya ziara hiyo, tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Simba kilikuwa; Juma Kaseja, Miraj Adam, Paul Ngalema, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Haroun Chanongo, Abdallah Seseme, Abdallah Juma/Rashid Ismail, Mrisho Ngassa/Marcel Kaheza na Kiggi Makassy/Amri Kiemba.
REKODI YA PATRICK LIEWIG SIMBA SC
Simba SC 4-2 Jamhuri (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 1-1 Tusker FC (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 1-1 Bandari (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 0-1 U23 Oman (Kirafiki)
Simba SC 1-3 Qaboos (Kirafiki)
Simba 2-1 Ahly Sidab (Kirafiki)

0 comments:

Post a Comment