.

.
Tuesday, January 29, 2013

11:29 PM
WATALII zaidi ya 100 kutoka nchi 25 ulimwenguni jana walianza safari yao ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuchangisha dola za Marekani zaidi ya milioni 1 sawa na zaidi ya sh bilioni 1.5 za Tanzania ambazo zitatumika kusaidia miradi ya wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi mbalimbali za taifa hapa nchini.
Safari hiyo imeandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini (Tanapa) kwa kushirikiana na kampuni ya Wings of Kilimanjaro ya nchini Australia ambapo watashuka toka kwenye kilele cha mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika kwa kuruka kwa kutumia miamvuli maalumu, tukio ambalo litakuwa ni la kwanza tangu kugunduliwa kwa mlima huo.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, meneja uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete, na meneja mradi wa kampuni hiyo, Adrian Mgrae, walisema kuwa fedha hizo zitaelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya kukabiliana na umaskini vijijini, uharibifu wa mazingira na misaada ya kibinadamu.
Walisema kuwa misaada hiyo inajumuisha uchimbaji wa visima vya maji safi ya kunywa, kuboresha miundo mbinu ya elimu na kusaidia waathirika wa virusi vinavyosababisha ukimwi inayosimamiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya One Foundation, Plant with Purpose na Worldsave International.
Walisema kuwa watalii hao wanaotarajiwa kupanda mlima huo kupitia njia ya Machame mwishoni mwa Januari, mwaka huu, wanatarajiwa kushuka kwa kuruka na miamvuli hiyo maalumu kati ya Februari 5 na 6 kulingana na hali ya hewa itakavyokuwa kwenye kilele cha Kibo.
Shelutete alisema kuwa watalii hao wanaotazamiwa kupanda mlima huo kwa muda wa siku saba wanatazamiwa kutua kwa miavuli hiyo kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Umbwe na Chuo cha Ufundi Stadi cha Kibosho, wilayani Moshi, hivyo aliwahimiza wananchi kujitokeza kujionea tukio hilo la kihistoria.
Meneja uhusiano huyo wa Tanapa alisema kuwa tukio hilo pia linatazamiwa kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 600 ambao watawahudumia watalii hao kwa safari ya kupanda milima huo ikijumuisha wabeba mizigo, wapishi na waongoza watalii.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya uwakala wa Utalii ya Top of Africa ya mjini Moshi, Silvanus Mvungi, ambaye ndiye aliyeandaa safari ya watalii hao alisema kuwa katika kuhakikisha usalama wa wageni hao kutakuwa na helikopta maalumu kwa ajili ya uokoaji ambayo itakuwa tayari muda wote mpaka kukamilika kwa shughuli hiyo.

0 comments:

Post a Comment