.

.
Monday, January 21, 2013

9:49 PM
 Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe (kulia) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam
 Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe (kulia) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam leo wakati akitangaza maamuzi yaliyofikiwa na Bodi ya Wakurugenzi juu ya shutuma mbalimbali za Viongozi wa Bandari. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu – Wizara ya Uchukuzi , John Mngodo  na katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mhandisi Omar Chambo.Picha Zote na Mdau Mroki.
 
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amewafukuza kazi vigogo watano wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kumrudisha mmoja kazini wakati mwingine akifanyiwa uchunguzi upya.
Valiotimuliwa ni Mkuruganzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe, naibu wake Hamad Konshuma, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Casian Nghamilo, Kapteni Tumaini Masalo na Julius Semfuko.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwakyembe alisema kuwa wanaendelea kumchunguza Kapten Lwakabale ambaye tuhuma zake bado hazijabainika wazi.
Mwakyembe amefikia uamuzi huo kufuatia ripoti iliyotolewa na tume ya uchunguzi iliyoundwa Agosti 27 mwaka jana, baada ya viongozi saba wa mamlaka hiyo kusimamishwa kazi kutokana na tuhuma za ufisadi.
Alisema kuwa tume ilifanya kazi ya kuchunguza huduma mbalimbali za bandari na kukabithi ripoti hiyo Oktoba mwaka jana. Vigogo hao walikutwa na makosa ya uzembe uliokithiri, kushindwa kudhibiti wizi, kukosa uaminifu kupindukia, matumizi mabaya ya madaraka na kukiuka sheria.
Alisema kuwa makosa hayo yamesababisha kushindwa kudhibiti kiwango cha utoaji mafuta machafu bandarini na kusababisha wizi wa mafuta masafi pamoja na kutoa kibali cha utoaji mafuta hayo kinyume na sheria.
Waziri Mwakyembe aliongeza kuwa vigogo hao kwa kushirikiana walitumia vibaya madaraka yao kwa kuingia mkataba na kampuni ya Kichina (China Communication Construction Company) bila idhini ya serikali pamoja na kupandisha mshahara kwa wafanyakazi wa bodi hiyo bila idhini ya waziri anayesimamia mamlaka hiyo.
Alifafanua kuwa makosa hayo yote hayakuleta faida yoyote katika kampuni hiyo zaidi ya kufukuza wateja na kusababisha hasara kubwa ambayo mpaka sasa bado kiasi chake hakijajulikana.
Katika ripoti hiyo, Mwakyembe alisema kwa sasa bandari ya Dar es Salaam ni ya mwisho kwa utendaji kati ya bandari 36 Afrika, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na DANIDA na Benki ya Dunia.
Alisema kuwa uamuzi huo ni wa awali na tume bado inaendela kufanya kazi yake. Na kuongeza kuwa amemrudisha kazini mhandisi Emmanuel Matala baada ya kuona hana makosa.
Katika hatua nyingine, Mwakyembe alishindwa kubainisha ni hatua zipi kisheria zitafuata baada ya kuwafukuza kazi.
 

0 comments:

Post a Comment