.

.
Monday, January 21, 2013

9:37 PM
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mh. Edward Lowassa 
 
MWENYEKITI wa Kamati Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowasa, ameeleza kushtushwa na wingi wa vijana gerezani na mahabusu na kusema kuwa hiyo ni hatari kwa uchumi wa nchi.
Lowasa alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati kamati yake ilipokutana na viongozi wa Jeshi la Polisi, magereza na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ujumla kwa ajili ya kujadili udhaifu ulioko kwenye magereza.
Alisema katika ziara ya kamati yake hivi karibuni ya kutembelea magereza mbalimbali nchini alibaini kwamba asilimia 90 ya vijana ndiyo waliojazana katika magereza kama wafungwa na mahabusu na kusema tatizo linachangiwa na ukosefu wa ajira.
Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alisema wajumbe wa kamati yake katika ziara hiyo walibaini udhaifu mkubwa katika utendaji kazi kati ya idara ya upelelezi, magereza na jeshi la polisi na kutaka viongozi wa juu kulishuighulikia suala hilo.
Alisema katika gereza la Segerea walibaini kuwa lilikuwa na mahabusu zaidi ya uwezo wake kwa asilimia 23, kwani lina wafungwa 98 na mahabusu 2,400.
“Hali hii inaitia aibu nchi yetu katika vyombo vya kimataifa vinavyotetea haki za binadamu, kwa sababu makosa mengi yanayosababisha mlundikano huo wa mahabusu ndani ya magereza ni makosa ya kijinga kabisa kama vile kuiba kuku, baiskeli, kuzurura au kupiga kelele,” alisema.
Aliongeza kuwa wamebaini kuwapo uonevu kwa wanawake, alitoa mfano kwa mahabusu mwanamke aliyewaeleza alikamatwa kwa kosa la kuzurura wakati alikuwa ametumwa dukani na mumewe kununua dawa na kwamba wakati anakamatwa alijitetea na mumewe lakini polisi waliomkata walimng’ang’ania na kumtaka alipe faini ya sh 200,000.
Wakati huohuo, Kamati ya Kudumu ya Mashirika ya Umma (POAC) imeurejesha ujumbe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili urekebishe hesabu za taasisi hiyo kwa miaka minne ya fedha tangu 2008 hadi mwaka 20011 pamoja na makosa mengine zaidi ya 25.
Pamoja na UDSM, pia wamemtaka Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanyia ukaguzi sh milioni 317 za Taasisi ya Mimea Nchini (TPRI) za mwaka wa fedha 2011/2012 ambazo zinadaiwa kupelekwa katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo.

0 comments:

Post a Comment